Aug 09, 2022 10:08 UTC
  • Sataliti ya Iran yarushwa anga za mbali kwa kutumia Roketi la Russia

Satalaiti ya Iran ya Khayyam imerushwa katika anga za mbali kwa kutumia roketi la Russia la Soyuz-2.1b ikiwa ni hatua mpya ya uhusiano wa kistratijia baina ya Tehran na Moscow katika masuala ya anga za mbali.

Satalaiti ya Khayyam imefikishwa katika anga za mbali kwa roketi hilo la Russia ambalo nalo limerushwa kutokea Kituo cha Baikonour Cosmordome nchini Kazakhstan ambacho kinasimamiwa na Russia.

Kwa mujibu wa taarifa, Satalaiti ya Khayyam itatumika katika kuchunguza mipaka ya Iran na kuimarishwa uwezo wa nchi katika sekta za kilimo, usimamizi wa mali asili, mazingira,  uchimbaji madini na kukabiliana na maafa ya kimaumbile.

Katika taarifa Shirika la Anga za Mbali (ISA) la Iran limekanusha ripoti kuwa Russia inalenga kutumia taarifa za sataliti hiyo kwa muda katika mgogoro unaoendelea sasa nchini Ukraine.

Taarifa hiyo imesema haiwezekani kwa nchi zingine au yeyote yule kupata taarifa za satalaiti hiyo isipokuwa Iran kwani ina alama za siri za algorithim ambazo zimetayarishwa na wataalamu wa ISA.

Kauli hiyo ya ISA imekuja baada ya gazeti la Kimarekani la Washington Post kudai kuwa sataliti ya Khayyam ya Iran itatumika kuisaidia Russia katika vita nchini Ukraine.

Satalaiti ya Khayyam ikiwa inaelekea katika anga za mbali

Satalaiti hiyo imepewa jina la Abu l-Fath Omar ibn Ibrahim Khayyam Nishapuri ambaye alikuwa mwanafalsafa, mwanahisabati, tabibu, malenga na mwandishi mkubwa wa Kiirani aliyeishi mwishoni mwa karne ya tano na mwanzoni mwa karne ya sita Hijria.

Katika miaka ya hivi karibuni Iran imechukua hatua kubwa katika uga wa teknolojia pamoja na kuwa inakabiliwa na vikwazo shadidi vya Marekani.

Mapema mwaka huu Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilirusha satalaiti yake ya pili katika eneo la anga za mbali linalojulikana kitaalamu kama LEO ikiwa ni miaka miwili baada ya kutuma satalaiti yake ya kwanza ya kijeshi katika anga za mbali.