Aug 10, 2022 01:30 UTC
  • Satalaiti ya Khayyam; hatua muhimu katika harakati ya Iran ya kuzitumia anga za mbali

Waziri wa Habari na Mawasiliano na Teknolojia wa Iran Issa Zarepour ametangaza kuwa satalaiti ya Kiirani ya Khayyam jana Jumanne ilipaa kuelekea anga za mbali umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini.

Zarepour ambaye alikuwa ziarani nchini Kazakhstan ametuma video kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram na kueleza kwamba, satalaiti ya Iran ya Khayyam ikiwa na bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeunganishwa na roketi la kubebea satalaiti la Soyuz na ilitazamiwa kurushwa kuelekea anga za mbali katika kituo cha anga za mbali cha Baikonur Cosmodrome nchini Kazakhstan mnamo saa saba na nusu mchana kwa wakati wa Tehran.

Zarepour amebainisha kuwa, hivi sasa Iran inao uwezo wa kuweka kwenye mzingo satalaiti nyepesi na kwamba satalaiti ya Khayyam, ambayo ina uzito wa kilogramu 600 itawekwa kwenye mzingo ulioko umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini. Satalaiti hiyo itatumika kwa ajili ya kuipatia Iran data na taarifa za anga za mbali inazohitaji, ikiwa ni hatua kubwa sana kwa taifa hili. Picha zenye umakini mkubwa zitakazotumwa na satalaiti hiyo zitaweza kutumiwa kuboresha matumizi ya anga za mbali ya Iran katika nyuga za hifadhi ya mazingira na kilimo.

Issa Zarepour

 

Utaalamu wa anga za mbali ni miongoni mwa teknolojia za kisasa. Licha ya vizuizi vya kila upande ilivyowekewa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuwa na utaalamu kamili wa teknolojia hiyo, ambapo katika miongo minne iliyopita imeweza kupiga hatua kubwa na za mtawalia katika teknolojia ya anga za mbali. Hivi sasa Iran ni moja ya nchi 10 zinazoongoza katika teknolojia ya anga za mbali, ambayo ni matunda na matokeo ya bidii na juhudi kubwa za muda wa miongo minne zilizofanywa na wataalamu wa humu nchini. Ni kwa sababu hiyo, Iran imeweza kupiga hatua na kuwa na nafasi maalumu katika utaalamu wa anga za mbali kati ya nchi chache zinazomiliki teknolojia hiyo. Kwa hivi sasa kuna nchi sita zenye utaalamu wa kuunda vituo vya kurushia satalaiti na Iran inatazamiwa kushika nafasi inayofuatia katika uundaji wa vituo hivyo.

Hata kama maadui wamejaribu kutumia vikwazo vya aina tofauti kukwamisha maendeleo ya kiuchumi na kisayansi ya Iran yakiwemo ya teknolojia ya anga za mbali, lakini licha ya mashinikizo na vizuizi vyote hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kupiga hatua katika teknolojia mbalimbali za anga za mbali, ambayo yanahesabika kuwa ni mafanikio makubwa kwa Iran ya Kiislamu. Kimsingi hasa ni kwamba, tofauti iliyopo kati ya Iran na nchi zingine za eneo la Asia Magharibi ni kuwa Iran inategemea uwezo wake wa ndani na inatumia vipaji vya wataalamu wake yenyewe kunufaika na teknolojia hiyo ya anga za mbali.

Satalaiti ya Iran ya Omidi

 

Kwa kutilia maanani nafasi na mchango muhimu wa satalaiti katika zama hizi kwenye nyuga zote zikiwemo za mawasiliano, habari, ugunduzi, ujasusi, mazingira na masuala mengi mengine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kwa dhati kustawisha miundomsingi na teknolojia yake ya makombora na anga za mbali na imeweza kupiga hatua na kupata maendeleo makubwa katika uga huo. Kubuni na kuunda maroketi ya kubebea makombora pamoja na hatua muhimu zilizopigwa katika utengezaji wa satalaiti zinazotokana na utaalamu wa ndani, urushaji wake, upokeaji data na taarifa na hatimaye utumiaji wa data hizo, ni mfumo kamili wa teknolojia hiyo ya anga za mbali.

Hili limekuwa jambo lisiloweza kukubalika wala kuvumilika kwa Marekani na utawala wa Kizayuni; na ndio maana Washington inafanya kila iwezalo kuzuia na kukwamisha maendeleo inayopata Iran katika anga za mbali. Hata hivyo ujuzi wa teknolojia ya anga za mbali wa Iran umetokana na utaalamu wa wanasayansi wa ndani; kwa sababu hiyo teknolojia hiyo inazidi kukua na kupiga hatua kubwa zaidi licha ya mashinikizo na vikwazo vya Marekani pamoja na upinzani wa Wamagharibi.

Waziri wa habari na mawasiliano ya teknolojia wa Iran anasema: Iran imeweza katika kilele cha vikwazo, tabu na misukosuko kufikia kwenye utalaamu wa juu kabisa katika uga wa anga za mbali, kiasi kwamba imeweza kufanikisha uundaji wa satalaiti na roketi la kuibebea, ambao unahitaji umakini wa hali ya juu ili kuufikisha kwenye mzingo uliokusudiwa.

Satalaiti ya Khayyam

 

Kwa sasa, kurushwa satalaiti ya Kiirani ya Khayyam ambako kumefanyika kwa kutumia roketi la Kirusi kunachukuliwa kama mwanzo wa ushirikiano wa kistratejia baina ya Tehran na Moscow katika sekta ya anga za mbali. Lakini pamoja na hayo waziri wa habari na mawasiliano ya teknolojia wa Iran amesema, sambamba na mashirikiano ya kistratejia yanayofanyika baina ya Iran nchi zinazotajika duniani katika teknolojia ya anga za mbali kama Russia, kustawisha teknolojia ya ndani ya utaalamu kunaendelea kupewa kipaumbele; na hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu litaweza kufikiwa lengo la kutuma satalaiti ya uchukuaji vipimo katika mzingo wa kilomita 500 wa anga za mbali.../

 

Tags