Aug 10, 2022 11:24 UTC
  • Wairani waandamana kulaani ukatili wa Israel dhidi ya wakazi wa Gaza

Wananchi wa Iran jana Jumanne walifanya maandamano katika mji mkuu Tehran kulaani jinai za utawala wa Kizayuni za kuwaua shahidi wanawake na watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.

Maelfu ya waandamanaji walioshiriki kwenye maandamano hayo walikusanyika katika Medani ya Palestina jijini Tehran, karibu na ubalozi wa Palestina hapa nchini, huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina na makundi ya muqawama.

Aidha waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kulaani ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza wasio na ulinzi.

Waandamanaji hao walisikika wakipiga nara za 'Mauti kwa Israel', 'Mauti kwa Wazayuni' na 'Mauti kwa Uingereza' huku wakitangaza uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Akiuhutubia umati mkubwa wa waandamanaji hao, Khalid Qaddoumi, Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema, "Maadui Wazayuni ambao wamewaua raia wasio na hatia, wanapaswa kushtakiwa katika mahakama za kimataifa za haki za binadamu, na wapewe adhabu kali."

Unyama wa Wazayuni Gaza

Takwimu za Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza zinaonesha kuwa, idadi ya Wapalestina waliouwa shahidi katika hujuma za kikatili za utawala haramu wa Israel tokea Ijumaa iliyopita ni watu 45 wakiwemo watoto wadogo 15, huku wengine karibu 400 wakijeruhiwa.

Hata hivyo utawala haramu wa Israel umelazimika kuafiki makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza baada ya kukabiliwa vikali na makombora ya mrengo wa muqawama. 

Tags