Aug 10, 2022 11:26 UTC
  • Raisi: Kuzinduliwa satalaiti ya Khayyam ni fahari kwa Iran

Rais wa Iran amesema kurushwa katika anga za mbali kwa mafanikio satalaiti ya Iran ya Khayyam ni chemichemi ya fahari na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema hayo mapema leo Jumatano katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa, karibuni hivi taifa hili litashuhudia mafanikio makubwa katika anga za mbali.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, kuanza kupokea data muhimu kutoka kwenye satalaiti hiyo iliyoundwa na wataalamu wa humu nchini ni fahari kubwa isiyo na kifani kwa taifa hili la Kiislamu.

Hapo jana Jumanne, Tehran ilitangaza kuwa, satalaiti ya Kiirani ya Khayyam ilipaa kuelekea anga za mbali umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini kwa mafanikio.

Khayyam

Satalaiti ya Khayyam imefikishwa katika anga za mbali kwa roketi la Russia lililorushwa tokea kwenye Kituo cha Baikonour Cosmordome nchini Kazakhstan ambacho kinasimamiwa na Russia.

Kwengineko katika hotuba yake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameienzi siku ya kuwakumbuka walinzi wa Haram Tukufu ambayo iliadhimishwa hapa nchini jana Jumanne Agosti 9.

Tags