Aug 11, 2022 07:24 UTC
  • Iran yajitenga na madai ya kijuba ya kutaka kumuua Bolton

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepinga madai ya kiwendawazimu na yasiyo na msingi yaliyotolewa na serikali ya Washington ikidai kuwa raia mmoja wa nchi hii alikula njama ya kumuua John Bolton, mshauri wa zamani wa Usalama wa Kitaifa wa Ikulu ya White House ya Marekani.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuibua tuhuma na madai yasiyo na msingi wala mashiko yoyote ni jambo la kawaida katika mfumo wa mahakama na propaganda za Marekani. 

Amesema: Katika kuendeleza sera iliyofeli ya kueneza chuki dhidi ya Iran, na hatua zisizokoma za kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu, Wizara ya Sheria ya Marekani imebuni hadithi mpya na kuibua madai pasi na kutoa ushahidi wowote.

Kan'ani amesisitiza kuwa, madai hayo ya urongo na yasiyo na msingi yametolewa na maafisa wa Marekani kwa malengo ghalati ya kisiasa.

Wizara ya Sheria ya Marekani jana Jumatano ilidai kuwa imemshitaki Shahram Poursafi kwa kujaribu kula njama za kumuua Bolton, kama jibu la mauaji ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Bolton katika enzi za Trump madarakani

Hii ni katika hali ambayo, mwezi Julai mwaka huu, Bolton alikiri kushiriki katika mipango na njama za mapinduzi dhidi ya serikali za nchi tofauti duniani.

Bolton ambaye alikuwa Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Donald Trump tokea 2018 hadi 2019, alikiri kwamba katika kipindi chake, aliunga mkono na kushiriki vilivyo katika mipango ya kuimarisha sera za uingiliaji na uhasama wa Marekani dhidi ya nchi nyingi duniani na hasa za Amerika ya Latini kama Bolivia, Cuba na Venezuela na Iraq katika Asia Magharibi.

 

Tags