Aug 11, 2022 10:49 UTC
  • Iran yaitaka Marekani kukubali matakwa halali ya Jamhuri ya Kiislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ameitaka Marekani kuandaa mazingira ya kuafikiwa rasimu ya mwisho ya makubaliano ya mazungumzo ya Vienna kwa kukubali "matakwa halali" ya Jamhuri ya Kiislamu.

Amir-Abdollahian aliyasema hayo Jumatano jioni katika manzungumzo na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavosoglu na kuongeza kuwa: "Tumefikisha ujumbe wetu kwa Marekani kupitia nchi za Ulaya. Tunatumai kuwa upande wa Marekani, iwapo utakuwa na mtazamo wa kihalisi na wa kimatendo na kukubali matakwa halali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, utatoa msingi wa makubaliano juu ya maandishi ya mwisho."

Mazungumzo kati ya Iran na nchi za Ulaya pamoja na Russia na China kwa ajili ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya 2015 kwa kuondoa vikwazo vya Marekani dhidi ya Tehran yamekuwa yakiendelea tangu Aprili 2021. Wakati utawala wa Rais Joe Biden umedai kuwa Marekani iko tayari kurejea katika mazungumo kwa kuzingatia makubaliano ambayo mtangulizi wake alijiondoa mnamo 2018, lakini bado haujachukua hatua zozote za kutengua makosa ya zamani ya Washington.

Siku ya Jumatatu, afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya Iran alipuuzilia mbali ripoti za vyombo vya habari vya Marekani kwamba maandishi ya kurejesha makubaliano na Iran yamekamilika na kwamba mazungumzo ya Vienna yamekamilika.

Mazungumzo ya Vienna

Maafisa wa Iran wamesema tayari wamewasilisha jibu la awali kwa rasimu hiyo na watarejea na maoni ya ziada baadaye.

Tovuti ya Nournews yenye mfungamano na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran imesema Jamhuri ya Kiislamu imetangaza wazi tokea awali kwamba haitatia saini mapatano hadi iwe na uhakika wa makubaliano juu ya masuala yote yaliyojadiliwa yatakayohakikisha maslahi ya taifa la Iran yanazingatiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Cavosoglu ameelezea matumaini kwamba mazungumzo ya sasa yatafikia tamati hivi karibuni ili kupatikana haki za taifa la Iran na maslahi ya pamoja ya pande zote.