Aug 12, 2022 03:09 UTC
  • Jibu la Kiongozi Muadhamu kwa Barua ya Katibu Mkuu wa Jihad Islami ya Palestina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu barua ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na kusema, "mapambano (muqawama) ya kishujaa ya Jihad Islami yatapelekea kupanda hadhi ya harakati hii katika mapambano sambamba na kusambaratisha hadaa za utawala wa Kizayuni na kuufedhehesha utawala huo."

Kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kujibu barua ya Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema, matukio ya hivi karibuni yameongeza fahari ya Harakati ya Jihad Islami na kuinua hadhi ya harakati hii miongoni mwa harakati  zingine shupavu za mapambano ya taifa la Palestina. 

Aidha amemuomba Mwenyezi Mungu alijaalie ushindi  wa karibu taifa lenye fahari na linalodhulumiwa la Palestina.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, nara zote za makundi ya Palestina katika ardhi zote za Palestina zinapaswa kuhimiza kulinda mashikamano na kuongeza kuwa: "Adui ghasibu anaendelea kudhoofika na harakati za mapambano ya Palestina zinaendelea kupata nguvu na sisi tunaendelea kuwa pamoja nanyi."

Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami hivi karibuni katika barua kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kushiriki kwa wingi na kishujaa Mujahidina wa Palestina, hasa Harakati ya Jihad Islami na tawi lake la kijeshi, Brigedi za Quds, kote Palestina na hasa Gaza na Ukingo wa Magharibi na kusema:"Kwa uwepo wa brigedi za mapambano ya Jihad haipiti hata siku moja katika Ukingo wa Magharibi bila kuwepo makabiliano na utawala wa Kizayuni."

Katibu Mkuu wa Jihad Islami ameashiria hali ya Gaza na kusema kusimama kidete eneo hilo mkabala wa utawala ghasibu wa Israel na huku akibainisha kuhusu mapigano ya siku tatu ya hivi karibuni amesema: "Mapigano hayo tuliayapa jina la 'Wahda al-Sahat'  (Mshikamano katika Medani) ikiwa ni njia ya kusisitiza umoja wa taifa letu katika kukabiliana na adui ambaye anatumia njama na nguvu zake zote kusambaratisha umoja huu."

Wapiganaji wa Jihad Islami

Ziad al-Nakhalah amesisitiza kuwa, katika vita hivyo maeneo yote ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (zilizopachikwa jina la Israel) yalikuwa katika upeo wa makombora ya Jihad Islami na kuongeza kuwa: "Mapigano hayo yalisambaratisha tathmini za utawala wa Kizayuni kiasi kwamba utawala huo ulilazimika kuomba usitishaji vita baada ya siku tatu tu na haukuwa na budi ila kukubali masharti ya muqawama."

Katibu Mkuu wa Jihad Islami amesema adui anafuatilia sera za kuibua mifarakano baina ya makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina na kuongeza kuwa: "Walitangaza lengo la vita lililikuwa ni kulenga Jihad Islami tu lakini Jihad Islami kwa muqawama na mapamabo yake shupavu  na ya kishujaa imeweza kuibua uungaji mkono na himaya ya vikosi vyote vya muqawama katika eneo na ulimwengu, na pia imeungwa mkono na taifa zima la Palestina na makundi  yote ya muqawama, yakiongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas."

Katibu Mkuu wa Jihad Islami ameyataja mafanikio hayo ya muqawama kuwa ni utangulizi wa ushindi mkubwa zaidi kwa taifa la Palestina katika siku zijazo na akashukuru nafasi ya harakati ya Hizbullah chini ya uongozi wa Seyed Hassan Nasrallah, pamoja na uungaji mkono na ridhaa ya Iran katika nyanja zote chini ya uongozi na muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katibu Mkuu wa Jihad Islami ya Palestina amesema bila ya uungaji mkono na kusimama  kidete bila kikomo Iran na Hizbullah, ushindi huu na ushindi uliopita haungepatikana.