Aug 13, 2022 01:32 UTC
  • Iran: Marekani haiwezi kuficha jinai zake kwa kuibua madai bandia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kitendo cha Marekani cha kuibua tuhuma na madai yasiyo na msingi wala mashiko yoyote hakiwezi kuficha wala kuhalalisha jinai za serikali ya Washington.

Nasser Kan'ani alisema hayo jana Ijumaa katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa Twitter na kueleza kuwa, Marekani imebuni tuhuma zisizo na msingi kwamba Iran imekula njama ya kutaka kumuua John Bolton, mshauri wa zamani wa Usalama wa Kitaifa wa Ikulu ya White House ya Marekani, ili kukwepa kuwajibishwa na jamii ya kimataifa kwa jinai zake.

Amebainisha kuwa, Marekani itaendelea kujipoteza itibari mbele ya macho ya Iran na dunia, ikiwa itaendelea kuyashupalia madai hayo bandia katika vyombo vya habari. 

Kan'ani amesema Washington inajaribu kumsafisha Bolton licha ya kuwa ni mwanasiasa aliyefilisika kimaadili, gaidi na mpangaji wa mapinduzi dhidi ya nchi na serikali huru duniani.

John Bolton

Wizara ya Sheria ya Marekani siku ya Jumatano ilidai kuwa imemshitaki Muirani, Shahram Poursafi kwa kujaribu kula njama za kumuua Bolton, eti kama jibu la mauaji ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Hii ni katika hali ambayo, mwezi Julai mwaka huu, Bolton alikiri kushiriki katika mipango na njama za mapinduzi dhidi ya serikali za nchi tofauti duniani, wakati wa utawala wa Donald Trump.

Tags