Aug 13, 2022 11:11 UTC
  • Marandi: Matukio kuhusu Bolton na Salman Rushdie yanatia shaka

Mshauri wa timu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo huko Vienna ameshangazwa na sadfa ya matukio mawili ya hivi karibuni huko Marekani, na kuashiria kuwa yumkini matukio hayo yanafungamana na mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mohammad Marandi amesema, madai ya Washington ya kuwepo njama ya kuuawa John Bolton na kushambuliwa mwandishi murtadi Salman Rushdie mjini New York; sambamba na kukaribia kufikiwa makubaliano kwenye mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa Iran huko Vienna, Austria, ni matukio yanayoshangaza.

Katika ujumbe kwenye Twitter, Marandi ameandika: Je haikushangazi kwamba wakati huu wa kuwepo uwezekano wa kufikiwa mapatano ya nyuklia, Marekani inaibua madai ya kutaka kuuawa Bolton, na kisha hili (kushambuliwa Rushie) linafanyika?"

John Bolton enzi za Donald Trump

Marandi ambaye pia ni mchambuzi mwandamizi wa masuala ya kisiasa na mitaala kuhusu Marekani katika Chuo Kikuu cha Tehran amesema binafsi hatadondosha machozi kumlilia mwandishi huyo aliyedhihirisha chuki zisizo na kikomo na dharau kwa Uislamu na Waislamu.

Mtaalamu huyo wa masuala ya kisiasa amemtaja Rushdie kama kibaraka cha mabeberu anayejidai kuwa ni mwandishi wa riyawa wa enzi za baada ya ukoloni.

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo ulirejea nchini hivi karibuni baada ya kumalizika duru ya sasa ya mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Vienna, tokea Agosti 4.

Mwandishi murtadi aliyeshambuliwa New York, Marekani

Ikumbukwe kuwa, Wizara ya Sheria ya Marekani Jumatano iliyopita ilidai kuwa imemshitaki Muirani, Shahram Poursafi kwa kula njama za kumuua Bolton, eti kama jibu la mauaji ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Hapo jana, Salman Rushdie, mwandishi murtadi wa kitabu cha Aya za Shetani kinachomtusi na kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW, alishambuiwa kwa kuchomwa kisu mjini New York Marekani, na hivi sasa yupo katika hali mahututi.

Tags