Aug 14, 2022 03:01 UTC
  • Abdollahian: Lugha ya vitisho dhidi ya Iran haitaambulia chochote

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani inapaswa kufahamu kuwa, kutumia lugha ya vitisho dhidi ya taifa la Iran hakutakuwa na manufaa yoyote kwa Washington.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa, "Historia inapaswa kuifunza Marekani kwamba, kutumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran na Wairani hakutazaa matunda yoyote."

Amesisitiza kuwa, kujaribu kupotosha mambo hakutaifanya Marekani isibebe dhima ya (mauaji ya) maelfu ya Wairani na wahanga wengine kwa kuhusika kwake na jinai za kigaidi katika eneo hili la Asia Magharibi.

Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa, taifa hili limeishi chini ya vitisho na vikwazo kwa miaka mingi na hata kupata mafanikio makubwa chini ya mashinikizo hayo, na kwa msingi huo, lugha ya heshima inapaswa kuchukua nafasi ya lugha ya vikwazo na vitisho.

John Bolton

Matamshi ya Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanaonekana kuwa jibu kwa madai ya kipropaganda ya Washington kwamba Iran imekula njama za kumuua John Bolton, mshauri wa zamani wa Usalama wa Kitaifa wa Ikulu ya White House ya Marekani, eti kama jibu la mauaji ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kitendo cha Marekani cha kuibua tuhuma na madai hayo yasiyo na msingi wala mashiko yoyote hakiwezi kuficha wala kuhalalisha jinai za serikali ya Washington.

Tags