Aug 14, 2022 07:30 UTC
  • Kani: Israel inakoseshwa usingizi na kizazi kipya cha Wapalestina

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema kuwaua watoto wa Kipalestina kumegeuka na kuwa jambo la kawaida kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, na umwagaji damu huo unadhihirisha wazi kuwa Wazayuni wanakiogopa kizazi kipya cha Wapalestina.

Ali Bagheri Kani alisema hayo jana hapa Tehran katika mazungumzo yake na Mohammed bin Abdulaziz al-Khulaifi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar anayesimamia masuala ya kieneo na kuongeza kuwa, "Mauaji ya watoto limekuwa jambo la kawaida kwa utawala wa Kizayuni, na hilo linaonesha kuwa Wazayuni wanahofia mustakabali wao."

 Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesisitiza kuwa, Palestina inasalia kuwa kadhia kuu katika umma wa Kiislamu, huku akitoa mwito kwa serikali za Kiislamu kuimarisha uungaji mkono wao kwa Wapalestina katika kila uga.

Mashahidi 15 kati ya 43 wa mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza walikuwa watoto, na takwimu rasmi sasa zinaonyesha kuwa jumla ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi na Israel tangu mwaka 2008 imefikia zaidi ya elfu moja.

Baadhi ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi na Wazayuni majuzi huko Gaza

Utawala wa Israel unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu umekuwa ukiuzingira Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya miaka 15, na kizazi kizima cha watoto wa Kipalestina kimeishi chini ya kivuli cha mzingiro huo wa kinyama.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amebainisha kuwa, mauaji dhidi ya watoto yanapaswa kulaani na jamii yote ya wanadamu na katika viwango vyote.

Wanadiplomasia hao wa Iran na Qatar wamejadili pia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Doha katika nyuga mbalimbali, mbali na kugusia mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Tags