Aug 14, 2022 11:30 UTC
  • Ghalibaf: Muqawama wa Palestina umetoa bishara ya kuangamia utawala wa Kizayuni

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, muqawama na mapambano ya harakati ya Jihad al Islami ya Palestina mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel yametoa bishara njema ya kuangamia utawala huo pandikizi.

Shirika la habari la IRNA limemnkuu Mohammad Bagher Ghalibaf akisema hayo leo katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran. Aidha amegusia muqawama na mapambano ya makundi mbalimbali ya Palestina na kusisitiza kuwa, harakati ya Jihad al Islami imethibitisha kivitendo kuwa, sehemu yoyote ya muqawama wa Kiislamu inaweza peke yake kukabiliana na adui na kumpigisha magoti. Sasa hivi kuangamia adui ghasibu kumekaribia mno kutokana na imani, mapenzi na ushirikiano wa karibu mno wa makundi ya muqawama.

Ijumaa ya tarehe 5 Agosti, utawala wa Kizayuni ulianzisha mashambulio makubwa ya anga na mizinga dhidi ya maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza. Mashambulizi hayo ya kikatili yameua shahidi Wapalestina wasiopungua 45 wakiwemo watoto wadogo 15 na wanawake wawili. Zaidi ya Wapalestia 360 wamejeruhiwa katika jinai hiyo mpya ya Wazayuni huku 96 kati yao wakiwa ni watoto wadogo, 30 ni wanawake na 12 ni vikongwe na vizee.

Spika Mohammad Bagher Ghalibaf katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran

 

Lakini kama alivyosema Msemaji wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina kuhusu vita hivyo vya siku tatu vya Ghaza kwamba utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu umeemewa na haukutarajia kuwa Wapalestina wangeweza kujihami kiasi chote kile.

Wanamapambano wa Palestina walijibu jinai hiyo ya Wazayuni kwa kuitwanga miji na vitongoji vya Kizayuni kwa mamia ya makombora. Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni pamoja na uwanja wa ndege wa Ben Gurion pia ulipigwa kwa makumi ya makombora ya wanamapambano wa Palestina. Wazayuni 60 wamejeruhiwa na kuwahishwa hospitalini baada ya maeneo yao kutwangwa kwa makombora ya wanamapambano wa Palestina.

Tags