Aug 15, 2022 04:22 UTC
  • Ebrahim Raisi: Muqawama ndiyo njia pekee ya kutatua masuala ya Waislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiisllamu ya Iran amesema kuwa, muqawama na mapambano ndiyo njia pekee inayoweza kutatua masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Rais Ebrahim Raisi akisema hayo jana kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri la serikali yake na huku akigusia kutangazwa tarehe 22 Mordad kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia kuwa siku ya muqawama wa Kiislamu humu nchini amesema, uzoefu wa kihistoria wa taifa la Iran unaonesha kuwa, mataifa ya dunia wakati wowote yanapokabiliana na ubeberu na uistikbari hayawezi kamwe kufanikiwa ila kwa kutumia njia ya muqawama na kusimama imara.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, fikra ya muqawama ndiyo inayoweza kutatua masuala yote ya ulimwengu wa Kiislamu hasa kadhia ya Palestina. Aidha ameitumia fursa hiyo kumkumbuka kwa wema kamanda mkubwa wa muqawama, Luteni Jenerali Alhaj Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiisamu SEPAH na kuongeza kuwa, wapigania ukombozi wote katika eneo hili na duniani kwa ujumla wanashukuru na kuenzi mapambano na jihadi ya makamanda wa muqawama.

Shahid Luteni Jenerali Qassem Soleiman, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

 

Kabla ya hapo pia, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) naye alikuwa amenukuliwa akisema kuwa, muqawama na mapambano ya harakati ya Jihad al Islami ya Palestina mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel yametoa bishara njema ya kuangamia utawala huo pandikizi.

Mohammad Bagher Ghalibaf alisema hayo jana katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran na kuongeza kuwa, sasa hivi kuangamia adui ghasibu kumekaribia mno kutokana na imani, mapenzi na ushirikiano wa karibu mno wa makundi ya muqawama.