Aug 15, 2022 07:06 UTC
  • Iran: Muqawama wa Kiislamu hauishii tu katika ukanda wa Asia Magharibi

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, muqawama na mapambano ya Kiislamu si kitu cha kuishia kwenye eneo moja tu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA,  Ali Bahadori Jahromi alisema hayo jana kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram kwa mnasaba wa tarehe 23 Mordad kwa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia ambayo ni Siku ya Muqawama wa Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa, leo ni Siku ya Muqawama wa Kiislamu.

Amesema: Kama katika miaka ya huko nyuma, Hizbullah ya Lebanon lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya siku 33, leo hii muqawama wa Ghaza unatumia siku tatu tu kuilazimisha Israel iombe kusimamishwa vita. Leo hii muqawama wa Kiislamu ni zaidi ya suala la eneo moja na hakuna anayeweza kukana na kufumbia macho nguvu zinazozidi kuongezeka za muqawama wa Kiislamu.

Ali Bahadori Jahromi

 

Msemaji huyo wa serikali ya Iran ameongeza kuwa, leo hii muqawama wa Kiislamu umetanua wigo wa eneo lake na kufika hadi Yemen, Iraq, Afghanistan, Syria na hata barani Afrika na Amerika ya Latini na kwamba mabeberu wa dunia hawapati usingizi katika sehemu yoyote ile. 

Inafaa kukumbusha hapa kwamba, siku kadhaa zilizopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliipongeza muqawama wa Palestina kwa kuushinda utawala wa Kizayuni kwa muda wa siku tatu tu na kusema katika sehemu moja ya miongozo yake ya busara kwamba: matukio ya hivi karibuni yameongeza fahari ya Harakati ya Jihad Islami na kuinua hadhi ya harakati hii miongoni mwa harakati nyingine shupavu za mapambano ya taifa la Palestina. Kwa muqawama wenu wa kishujaa, mumesambaratisha sera za  hadaa za utawala wa Kizayuni na kuufedhehesha utawala huo.  

Tags