Aug 15, 2022 12:27 UTC
  • Amir-Abdollahian: Leo tunakabidihi mapendekezo yetu ya mwisho katika JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, siku zijazo ni siku muhimu kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba Tehran inasubiri uamuzi kutoka upande wa Marekani kuhusu maudhui ya tatu.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo leo katika mkutano maalumu na waandishi wa habari wa masuala ya sera za nje, ambapo pamoja na mengine ametoa ufafanuzi kuhusu taarifa mpya za mazungumzo ya uondoaji vikwazo.

Amir-Abdollahian amesema, katika masuala ya kitaifa, pande zote nchini zina mtazamo mmoja; na mirengo yote ya kushoto na kulia huwa inaunga mkono maslahi ya taifa, jambo ambalo limeitia nguvu timu ya Iran katika meza ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongezea kwa kusema: katika mazungumzo yumkini yakakuwepo matatizo kadhaa, kwa hiyo makubaliano yanayofikiwa ni matokeo ya mapatano baina ya nchi saba na katika matini inayopitishwa, Iran inaweza ikawa sehemu ya wapitishaji wa matini hiyo.

 

Pamoja na hayo Amir-Abdollahian amesistiza kwa kusema: "endapo mistari yetu myekundu itazingatiwa, sisi hatuna tatizo juu ya kufikia makubaliano; na moja ya sababu za mazungumzo kuchukua muda mrefu ni kwamba hatutaki kuivuka mistari myekundu."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha pia kuwa, "upande wa Marekani umeeleza kwa maneno kwamba umekubaliana na maudhui zetu mbili, kwa hiyo tunasubiri jibu la maudhui ya tatu; na hadi ifikapo saa sita usiku wa leo tutatuma kimaandishi mapendekezo yetu ya mwisho kwa mratibu wa Umoja wa Ulaya katika JCPOA.../ 

Tags