Aug 16, 2022 07:50 UTC
  • Jeshi la Majini la Iran kufanya operesheni maalumu mwaka huu

Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran amesema vikosi vya baharini vya nchi hii vimejiandaa kikamilifu kufanya operesheni katika bahari yoyote ile duniani, na kwamba vinajiandaa kufanya operesheni maalumu kabla ya kumalizika mwaka huu wa Kiirani unaoisha Julai 22 mwaka 2023.

Admeri Shahram Irani amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Fars New na kuongeza kuwa, "Tarehe ya operesheni hiyo maalumu inategemea mipango ya makao makuu (ya Jeshi la Majini) lakini bila shaka itafanyika mwaka huu (wa Hijria Shamsia)."

Kamanda huyo amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia ukweli kwamba Jeshi la Majini la Iran lazima liwe na vikosi katika bahari zote duniani, limeazimia kuunda meli kadhaa ambazo zitakuwa kambi za kuelea baharini za vikosi hivyo.

Admeri Irani ameeleza bayana kuwa, uzalishaji wa meli za aina hiyo ni jambo la dharura kwa taifa hili, na anatumai kuwa manowari hizo zitazalishwa karibuni.

Manowari ya jeshi la majini la Iran

Amekariri kuwa, Iran inafadhilisha amani na wala haitaki vita na maadui, lakini adui akitishia usalama wa nchi hii, basi vikosi vya Jeshi la Majini la Iran vipo tayari na vimejiandaa kutoa jibu mwafaka. 

Wiki iliyopita, Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilitangaza kuwa makomandoo wa jeshi hilo wamezima hujuma ya maharamia dhidi ya meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari Nyekundu.

Tags