Aug 16, 2022 14:27 UTC
  • Iran: Nchi zote zina haki ya kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya  amani

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema nchi zote zina haki ya kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na amesisitiza kuwa,Iran ina azma ya kuendelea kumiliki teknolojia hiyo pamoja na kuwepo mashinikizo na uhasama wa baadhi ya madola makubwa.

Mohammad Eslami amesema kumiliki teknolojia ya nyuklia  kwa mtumizi ya amani ni msingi halali wa nguvu na uwezo kwa nchi yoyote ile.

Eslami amesema baadhi ya madola makubwa yanatumia vibaya haki yao  ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuizuia Iran kuendeleza miradi yake ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Kwa mujibu wa Eslami, kumetolewa tuhuma kadhaa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa miaka mingi na hata faili lake la nyuklia limefikishwa katika Bodi ya Magavana wa IAEA na Baraza la Usalama jambo ambalo limepelekea Iran iwekewe  vikwazo.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran aidha amesema katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuwa akisisitiza umuhimu wa kustawisha teknlojia ya nyuklia.

Eslami amesema Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran lina mpango kamili wa kistratijia na limechukua hatua za kustawisha  zaidi teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani nchini.

Mwezi Februari Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema maadui wanalengo la kuipokonya Iran haki ya kutumia teknolojia ya nishati ya nyuklia huku akisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kufuatilia silaha za nyuklia.

Kauli ya Eslami imekuja masaa machache baada ya Iran kuukabidhi Umoja wa Ulaya mapendekezo yake ya mwisho kuhusu mazungumzo ya ngazi za juu ya Vienna yenye lengo la kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015.