Aug 17, 2022 09:15 UTC
  • Jibu la Iran kwa rasimu iliyopendekezwa na Umoja wa Ulaya

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekabidhi kwa mratibu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo jibu la maandishi kuhusiana na nakala rasmi ya rasimu ya mapatano ya Vienna.

Alipozungumza siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alisema: "leo usiku tutakabidhi kimaandishi mapendekezo yetu ya mwisho kwa mratibu wa Umoja wa Ulaya katika JCPOA" na akasisitiza pia kwa kusema: "Ikiwa jibu la Marekani litaendana na uhalisia wa mambo na kuwa tayari kubadilika kulingana na hali, mwafaka utafikiwa; la kama Marekani haitaonyesha mabadiliko itabidi tufanye mazungumzo zaidi."

Hossein Amir-Abdollahian

 

Amir-Abdollahian alifafanua zaidi kwa kueleza kwamba: katika mazungumzo ya karibuni ya Vienna, upande wa Marekani umeonyesha kubadilika kwa kiwango fulani kwa maelezo uliyotoa juu ya maudhui mbili, maelezo ya maneno ambayo inapasa yawekwe kwenye sura ya maandishi; na katika maudhui ya tatu ambayo inahusiana na suala la kuwepo dhamana na hakikisho, kuna ulazima wa kupatikana hakikisho la Marekani na mabadiliko yanayohitajika na yanayozingatia uhalisia wa mambo.

Hata hivyo Jumatatu hiyohiyo, Marekani ilikariri baadhi ya madai yake na kutumia tena mbinu ya kujivua na dhima na masuulia katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo. Katika mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price alisema: "njia pekee ya kurudi pande zote mbili kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran ni kwa Tehran kuweka kando matakwa ya nje ya JCPOA." Ajabu ni kwamba Price alitoa matamshi hayo bila kutilia maanani kwamba, kwa kuwa Marekani ndiye msababishaji wa hali iliyopo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA inapaswa ifidie gharama za makosa iliyofanya huko nyuma.

Ned Price

 

Viongozi wa Marekani wanajaribu kuonyesha kwamba Iran inadai mambo ya ziada ilhali masuala yanayohusu ukaguzi na usimamizi wa miradi yake ya nyuklia hayatenganishiki na JCPOA na wala wala hayawezi kudaiwa kuwa ni matakwa ya ziada ambayo Iran inadai, kwa sababu mwaka 2015 na katika hati ya makubaliano hayo ya nyuklia pande husika zilitoa ahadi ya kulifunga faili la madai dhidi ya mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Lakini pamoja na hayo na katika mwendelezo wa sera za Marekani zilizogonga mwamba za utoaji mashinikizo ya juu zaidi, Price alitishia kwa kusema, "ikiwa Iran haitaweza au haitakuwa na utayari wa kutekeleza kikamilifu JCPOA, sisi tuko tayari kuendelea kutekeleza kwa ukali zaidi vikwazo vyetu pamoja na kutumia mashinikizo mengine ya kidiplomasia."

Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alitangaza pia kuwa, nayo Washington kwa upande wake, itawasilisha jibu lake kuhusiana na rasimu ya makubaliano kwa mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya.

Joep Borrell

 

Kabla ya duru ya karibuni ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo iliyofanyika Agosti 4 mjini Vienna, mkuu wa sera za nje wa AU Josep Borrell alitangaza kuwa ameshaandaa hati ya rasimu ya kufufua Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Ulaya alidai kwamba, hati hiyo aliyotayarisha yeye ni "makubaliano bora kabisa yanayowezekana kufikiwa" na kwamba lazima maamuzi yachukuliwe sasa hivi.

Siku tano baada ya kutolewa kauli hiyo na Borrell, Ali Baqeri Kani, mjumbe mwandamizi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo alisisitiza kuwa, ujumbe wa Iran umewasilisha rai za mapendekezo yake kimuundo na kimatini kwa madhumuni ya kufungua njia itakayowezesha kufanywa majumuisho ya haraka ya mazungumzo. Kauli hiyo ilikuwa inamaanisha kwamba, upande wa Iran hautaburuzwa na rasimu iliyowasilishwa na nchi za Magharibi na kwamba makubaliano pekee ambayo utakuwa tayari kuyasaini ni yale yatakayo ihakikishia Iran manufaa ya kiuchumi yatokanayo na JCPOA.

Kama inavyojulikana, tokea mwanzo wa mazungumzo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa ikitangaza kila mara kuwa, iko tayari kufikia makubaliano endelevu, thabiti na ya kuaminika, lakini haitavuka mistari myekundu iliyowekwa na Mfumo wa Kiislamu. Na ili kuweza kufikia makubaliano, Tehran imewasilisha pia kwa upande wa pili katika mazungumzo mapendekezo na ubunifu unaotekelezeka; na hata imekuwa tayari kubadilika pia kulingana na hali. Kwa msingi huo, ikiwa serikali ya Marekani itashikiliia msimamo wake wa kuyakataa matakwa ya msingi na ya kimantiki ya Iran na kuendeleza pia sera iliyofeli ya utumiaji vikwazo, hiyo itatathminika kama ishara nyingine ya kuonyesha kuwa White House haina nia ya dhati na ya kweli ya kuhakikisha mwafaka unapatikana katika mazungumzo.

 

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, makubaliano yoyote yale yatakayofikiwa itapasa yapelekee kufutwa kila wenzo wa mashinikizo unaoweza kuja kutumiwa siku za usoni dhidi ya Iran. Vilevile yatoe hakikisho la kuwepo utaratibu thabiti na endelevu wa kuondolewa vikwazo na pia yalidhaminie taifa la Iran manufaa na maslahi yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema, siku zijazo zitakuwa siku muhimu kwa makubaliano ya nyuklia na akasisitiza kwa kusema: "ikiwa Marekani itaonyesha mabadiliko katika siku zijazo tutafikia makubaliano, lakini kama hitaonyesha pia, hautakuwa mwisho wa dunia; wao wanazungumzia mpango B, na sisi pia tunao mpango wetu B. Lakini tunaamini, suala hili inapasa lipatiwe mwafaka kupitia mazungumzo, kwa pande zote kuzingatia uhalisia wa mambo".../