Aug 18, 2022 03:43 UTC
  • Harakati ya Jihad Islami kuendeleza mapambano hadi ukombozi kamili wa Palestina

Afisa wa harakati ya mapambano ya Jihad Islami ya Palestina amesema mapambano na muqawama dhidi ya utawala vamizi na ghasibu wa Israel yataendelea hadi ukombozi wa ardhi zote za Palestina.

"Harakati ya Jihad ya Palestina itaendelea na mapambano," mwakilishi wa harakati hiyo nchini Iran Nasser Abu-Sharif alisema siku ya Jumatano, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Khaled al-Qaddumi, mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, nchini Iran, kuhusu mafanikio ya vita vya hivi karibuni kati ya Israel na harakati za muqawama na mapamabano ya ukombozi katika Ukanda wa Gaza.

"Lengo kuu halijafikiwa, na mapambano haya yataendelea hadi ukombozi kamili wa ardhi ya Palestina," amesema.

Abu-Sharif amebainisha kuwa kuuawa shahidi sio kikwazo kwa ukombozi wa ardhi ya Palestina.

Amesema namna muqawama na taifa la Palestina linavyojibu utawala wa Israel imebadilika katika miaka ya karibuni.

"Ni kweli kwamba tumepoteza makamanda wetu wawili waandamizi, Khaled al-Mansour na Tayseer al-Jabari, na hii ni hasara kubwa, lakini harakati ya Jihad ya Kiislami ya Palestina ni harakati iliyopangwa ambayo inaweza kuchukua nafasi ya makamanda hawa waliouawa shahidi," ameongeza.

Watoto Wapalestina waliouawa na jeshi la Israel katika vita vya Gaza

Abu-Sharif alikuwa akiashiria wimbi la mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yaliyoanza tarehe 5 Agosti na kudumu kwa siku tatu mfululizo, na kuua makumi ya watu, wakiwemo watoto 17 na wanachama wakuu wa Jihad Islami na mamia ya wengine pia walijeruhiwa wakati wa uvamizi huo wa Israel.

Katika kukabiliana na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, Jihad Islami ilivurumisha mamia ya makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, na kuufanya utawala wa Tel Aviv kukubali usitishaji vita uliosimamiwa na Misri.

Qaddumi kwa upande wake alisema harakati za muqawama au mapambano zitalipiza kisasi cha damu ya mashahidi wa Kipalestina. Aidha amewataka waandishi habari kuakisi zaidi jinai za utawala haramu wa Israel.