Aug 18, 2022 08:22 UTC
  • Kufanyika kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Pakistan mjini Islamabad

Kikao cha 21 cha Kamisheni ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Pakistan kilianza Jumatano ya jana katika mji mkuu wa Pakistan Islamabad ambapo ujumbe wa Iran katika kikao hicho unaongozwa na Rostam Qassemi, Waziri wa Barabara na Ujenzi wa Miji.

Katika kikao cha ufunguzi jana asubuhi, maafisa wa Iran na Pakistan walibainisha uhusiano mzuri na imara baina ya pande mbili katika akthari ya nyanja. Aidha wamesema kuwa, kufanyika kikao cha ushirikiano wa kiuchumi kunaweza sambamba na kuondoa vizingiti vilivyoko njiani, kukaandaa uwanja pia wa kuimarisha zaidi uhusiano wa Tehran na Islamabad katika uga wa kiuchumi na sekta nyingine.

Kikao cha mwisho kama hicho kilifanyika Aprili mwaka 2017 hapa mjini Tehran. Kuongezwa muda wa uhusiano wa kistratejia wa nchi mbili, kuboresha uhusiano wa kibiashara, kuimarisha biashara za mipakani kupitia kuanzisha na kufanya amilifu masoko ya mipakani sambamba na kuanzisha vitongoji vya viwanda vya pamoja katika maeneo ya mpakani ni miongoni mwa malengo ya kikao cha 21 cha Kamisheni ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Pakistan. Aidha masuala kama usafiri na uchuukuzi wa anga, reli, bahari, ushirikiano katika mawasiliano, elimu, utalii na masuala ya kimahakama yanatarajiwa kujadiliwa katika kikao hiki.

Kupanua mashirikiano ya kiuchumi na majirani na mataifa ya eneo ni miongoni mwa vipaumbele katika siasa za kigeni za serikali ya awamu ya 13 ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran chini ya uongozi wa Rais Ebrahim Raeisi. Ni kwa kuzingatia hilo, ndio maana maafisa wa Iran na Pakistan wametiliana saini hati tatu za ushirikiano katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, lengo likiwa ni kuinua mahusiano ya kibiashara. Kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara katika kipindi cha miaka mitano, ushirikiano wa maonyesho mbalimbali, kuongeza muda wa mpango wa miaka mitano wa ushirikiano wa kibiashara hadi mwaka 2027 sambamba na kuanzisha masoko madogo ya pamoja katika maeneo ya mpakani ni miongoni vya mambo yaliyomo katika hati hizo tatu za makubaliano.

 

Rais Ibrahim Raeisi, wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria katika mazungumzo yake kwa njia ya simu Julai 9 mwaka huu na Shahbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan kwamba, Tehran haina kikwazo na mpaka katika kupanua uhusiano wake na Islamabad. Ibrahim Raeisi aliongeza kuwa, kufanyika kwa mpangilio kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi ni jambo ambalo daima litaaanda uwanja wa kuinua kiwango cha ushirikiano wa nchi mbili hizi jirani.

Iran na Pakistan zina mpaka wa pamoja wenye urefu wa zaidi ya kilomita 900. Kwa msingii huo mataifa haya mawili yana daghadagha na wasiwasi mwingi wa pamoja. Nchi mbili hizi zina mambo mengi ya pamoja kama ya kidini, kiutamaduni, ada na desturi za pamoja. Aidha kutokana na kuwa ni mataifa jirani gharama za kibiashara kwa namna fulani ni ndogo na zinadhamini maslahi ya pande mbili.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kutokana na mataifa haya kuwa na maeneo ya mipakani yanayohitimishia safari za pande mbili, kuweko usafiri na uchukuzi baina ya mataifa haya mawili na masoko madogo katika maeneo ya mpakani ni fursa nzuri na mwafaka kwa ajili ya kusaidi kupanua ushirikiano wa pande mbili wa kiuchumi.

 

Katika fremu hiyo, mahusiano ya pande mbili ya Iran na Pakistan katika uga wa kiuchumi, masoko, biashara na mipaka yamepiga hatua kubwa na ya kuzingatiwa katika miaka ya hivi karibuni. Iran na Pakistan katika kipindi cha miaka miwili iliyopita zimechukua hatua za kufungua vivuko viwili vipya vya mpakani na hivyo kuvifanya vivuko rasmi vya mpakani kufikia vitatu ambapo moja ya malengo ya hilo ni kurahisisha biashara na kutumia uwezo wa kila mmoja kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wao wanaoishi mipakani.

Inatabiriiwa kwamba, katika kikao cha 21 cha Kamisheni ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Pakistan kutafanyika mazungumzo muhimu pia baina ya jumbe za pande mbili kwa ajili ya kuboresha zaidi hali ya ushirikiano na kuyafanya amilifu masoko ya mpakani sambamba na kurahisisha upelekaji na uingizaji wa bidhaa baina ya nchi mbili.

Hapana shaka kuwa, kukuzwa kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Iran na Pakistan kunaweza kuwa na taathira chanya katika kuimarisha mafungano na uhusiano wa nchi hizi mbili jirani za Kiislamu.