Aug 20, 2022 04:35 UTC
  •  Salami: Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umo mbioni kujizatiti kwa silaha dhidi ya Wazayuni

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema kuwa, mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel yamefika hadi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuongeza kuwa, hivi sasa eneo hilo limo mbioni kujizatiti kwa silaha kwa ajili ya kukabiliana na Wazayuni maghasibu.

Brigedia Jenerali Hussein Salami sambamba na kubainisha kwamba, harakati ya ukombozi wa Palestina imekuwa na kupata nguvu kwa kupita zama na imezidi kukomaa  na kueleza kwamba, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa Wazayuni wengi wameangamia katika operesheni za makundi ya muqawama katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Kamanda Salami, operesheni za mwaka huu za makundi ya wanamapambano wa Palestina dhidi ya Wazayuni maghasibu katu haziwezi kulinganishwa na za mwaka jana kwani zimeshika kasi na kuongezeka pakubwa.

 

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesisitiza kuwa, kuendelezwa jihadi ni jambo muhimu sana na kwamba, kama ambavyo eneo la Ukanda wa Gaza limejizatiti kwa silaha, kwa mbinu hiyo hiyo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nao unaweza kujizatiti kwa silaha na hali hii imo mbioni kujitokeza.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiisalamu ya Palestina HAMAS wamekuwa wakieleza kwamba, muqawama uko chini ya mwavuli wa uungaji mkono wa kivitendo wa Wapalestina na jambo hilo ndilo linalozidi kutia nguvu harakati za muqawama katika eneo laUkingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani na washirika wake umeshadidisha njama na hujuma dhidi ya Palestina; hata hivyo hadi sasa njama zake zimefeli.