Aug 29, 2022 07:29 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuzipa nchi nyingine uzoefu wetu wa kupambana na vikwazo kwa miongo minne

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuzipa nchi nyingine rafiki, uzoefu wake wa kukabiliana na vikwazo kwa zaidi ya miaka 40 na kuvigeuza vikwazo hivyo kuwa fursa ya maendeleo na kujitegemea kila upande.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kumnukuu Bw. Ali Bagheri Kani  akisema hayo jana Jumapili hapa mjini Tehran wakati alipoonana na Freddy Mamani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bolivia na kuongeza kuwa, Iran ina uzoefu mzuri sana wa kupambana na mashinikizo ya kigeni na iko tayari kuzipa nchi nyingine uzoefu wake wa zaidi ya miaka 40 wa kukabiliana na vikwazo hivyo na kuvigeuza kuwa fursa za kujiletea maendeleo, kuwa huru na kujitegemea katika nyuga zote.

Bagheri Kani amegusia pia nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuziokoa nchi za ukanda huu na janga baya la ugaidi na kusisitiza kuwa, leo hii muqawama umetoka katika sifa yake ya kuwa maneno na fikra tu na umekuwa ni kigezo kikubwa, cha pande zote na chenye manufaa mno kwa mataifa yanayopigania ukombozi.

Bw. Ali Bagheri Kani

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, utamaduni wa muqawama umekuwa na mchango mkubwa na muhimu na umegeuka kuwa ngao muhimu ya kiusalama na ni kwa sababu hiyo ndio maana lazima tukiri kuwa, kuweza baadhi ya nchi kulinda usalama wao wa ardhi nzima na kuokoka kwenye njama za kuzigawa vipande vipande kumetokana na aidiolojia hiyo ya muqawama iliyojikita katika safu za wananchi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bolivia amesema kuwa, nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuwa na uzoefu mzuri wa kushirikiana katika nyuga mbalimbali za kieneo na kimataifa na ametilia mkazo wajibu wa kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano huo.

Tags