Sep 06, 2022 02:15 UTC
  • Waziri wa Afya wa serikali ya Taliban ya Afghanistan yupo ziarani nchini Iran

Waziri wa Afya wa Serikali ya Taliban ya Afghanistan yupo ziarani hapa nchini Iran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa serikali hiyo.

Mara baada ya kuwasili hapa mjini Tehran, Qalandar Ibad amesema kuwa, nchi mbili za Iran na Afghanistan zina mambo mengi yanayoziunganisha na kwamba nchi yake inahitajia uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu katika upande wa tiba na matibabu.

Vile vile amesema, moja ya malengo ya safari yake hapa nchini Iran ni kupata uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu katika kutia nguvu ratiba za masomo kwa wananchi wa Afghanistan ambalo ni moja ya masuala muhimu sana hasa katika upande wa wataalamu wa afya na matibabu.

Hospitali ya Imam Khomeini (MA) katika mkoa wa Bamyan wa katikati mwa Afghanistan

 

Kabla ya kuja humu nchini, Waziri wa Afya wa Serikali ya Taliban ya Afghanistan alizungumza na balozi wa Iran mjini Kabul kuhusu kumaliziwa kujengwa hospitali ya mkoa wa Bamyan wa katikati mwa Afghanistan, kuwapa mafunzo ya matibabu wananchi wa Afghanistan katika vitengo vya saratani, na kupelekwa madawa na vifaa vya tiba vya Iran huko Afghanistan.

Mara kwa mara kundi la Taliban limekuwa likihimiza kuongezwa misaada y Iran kwa Afghanistan hasa katika kipindi hiki kigumu ambapo nchi hiyo ina maratizo mengi hasa ya kiuchumi kutokana na jamii ya kimataifa kutoonesha nia ya kuitambua rasmi serikali ya Taliban na kukataa kabisa kushirikiana nayo.

Maisha ya wananchi wa Afghanistan yamezidi kuwa mabaya, hususan baada ya kuingia madarakani kundi la Taliban na kutokubali kundi hilo kufuata masharti ya jamii ya kimataifa hasa kuunda serikali inayoshirikisha makundi yote ya kijamii na kikabila ya nchi hiyo.

Tags