Sep 14, 2022 07:55 UTC
  • Iran: Muafaka utapatikana Marekani ikizingatia uhalisia wa mambo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, ikiwa Marekani itazingatia uhalisia wa mambo, basi makubaliano mazuri, imara na ya kudumu yanaweza kufikiwa kwa uungaji mkono wa pande zote katika mazungumzo ya Vienna.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo mapema leo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria na kueleza kuwa, mafanikio ya mazungumzo hayo ya Vienna yatategemea irada ya upande wa pili na utayarifu wa kuliondolewa vikwazo vya kidhalimu taifa la Iran.

Amir-Abdollahian ameashiria hatua ya nchi za Magharibi ya kutoangalia mambo katika uhalisia wake na kubainisha kuwa, Iran inafanya juhudi zake zote kuhakikisha mazungumzo yanaendelea huko Vienna na yanafikia makubaliano ya mwisho.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, lengo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuhakikisha kuwa makubaliano yanayofikiwa yanakuwa thabiti na endelevu. Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ametilia mkazo kustawishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote akisema, hilo ni miongoni mwa mihimili mikuu katika sera za nje za serikali ya Iran.

Mazungumzo ya Vienna

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama ameashiria irada njema ya kisiasa iliyooneshwa na Iran katika kipindi chote cha mazungumzo ya Vienna na kusisitiza kuwa, nchi yake inaunga mkono kukamilishwa mazungumzo hayo kwa ajili ya kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran.

Amesema msingi wa kuimarika uhusiano wa pande mbili wa Iran na Nigeria umetokana na mafungamano ya kihistoria baina ya mataifa haya mawili, huku akieleza kuwa anatumai kuwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya Tehran na Abuja utapanuka na kuimarika zaidi.

Tags