Sep 21, 2022 08:26 UTC
  • Sura halisi ya Mapinduzi ya Kiislamu, sababu kuu ya vikwazo dhidi ya Iran

Alena Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amesambaza rasmi ripoti yake kuhusu athari za vikwazo vya Marekani kwa wananchi wa Iran na kusema kuwa, vikwazo hivyo vipo na vimeendelea kuwepo tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Douhan aliitembelea Iran kuanzia tarehe 17 hadi 28 Mei mwaka huu wa 2022 na kuona kwa karibu taathira hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani kwa wananchi wa Iran na hivi karibuni amesambaza rasmi ripoti yake kamili kuhusu athari hizo. Ripoti hiyo imeanggalia maeneo tofauti na moja ya maeneo hayo ni kutumiwa vikwazo kama silaha katika siasa za mambo ya nje

Vikwazo ni moja ya silaha kuu ambazo zimekuwa zikitumiwa na Marekani kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 44 iliyopita. Marekani imekuwa ikitumia visingizio tofauti katika kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiilamu ya Iran. Kitendo cha kiistikbari cha Marekani cha kuanza kuwawekea vikwazo wananchi wa Iran mara tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini ni ushahidi tosha kwamba Washington inatumia silaha hiyo kutokana na sura halisi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo yamelikomboa taifa hili na kulifanya lisikubali tena kuburuzwa.

Alena Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa

 

Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa muitifaki mkubwa wa nchi za Magharibi na ilikuwa ni moja ya nguzo kuu za kutekelezea siasa za Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Wakati huo Iran ilikuwa dhaifu kiasi kwamba haikuthubutu kuhoji amri zilizokuwa zinatolewa na madola ya Magharibi. Hata masuala ya kidini pia hayakuwa na nafasi kubwa katika siasa za Iran. Utawala wa wakati huo wa kifalme wa Iran ulikuwa hauna upinzani wowote kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hali hiyo imebadilika kikamilifu. Siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ni kuhakikisha taifa la Iran lina nguvu, ni imara, haliburuzwi na ni mtetezi mkuu wa wanyonge duniani. Masuala ya kidini yamekuwa na nafasi kubwa hivi sasa katika siasa za ndani na nje za Iran. Bila ya shaka siasa hizo mpya za Iran zinakinzana kikamilifu na sera za kibeberu za madola ya Magharibi. Siasa za Iran za kuwahami wanyonge wakiwemo wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina ni kikwazo kikubwa cha kufanikishwa siasa za kidhalimu na za kuingilia kati masuala ya mataifa mengine, zinazoendeshwa na madola ya kiistikbari.

Ukweli ni kuwa, Marekani haikutarajia kabisa kuiona Iran innageuka kuwa Jamhuri ya Kiislamu yenye nguvu na imara katika nyuga zote. Kwa hamaki zake, Marekani iliamua kulishinikiza kila upande taifa la Iran mara tu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini. Kiujumla hakuna uadui wowote ambao haujafanywa na Marekani dhidi ya taifa la Kiislamu la Iran. Katika ripoti yake, Alena Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema, awali vikwazo vilikuwa vinalenga sekta ya mafuta tu, lakini tangu mwaka 2010 vikwazo hivyo vimewekwa kwenye sekta nyingine zote za kiuchumi za Iran. Sababu kuu ya kutanuliwa wigo wa vikwazo hivyo dhidi ya Iran ni kutokana na maendeleo makubwa inayopata kila leo Jamhuri ya Kiislamu na kuimarika nguvu zake hasa katika eneo la Asia Magharibi.

Viikwazo vya Marekani havichagui, vinalenga mpaka dawa za wagonjwa wenye maradhi maalumu wa nchini Iran

 

Nukta nyingine muhimu katika ripoti ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa, Alena Douhan ni kwamba hivi sasa vikwazo vya madola ya kibeberu hasa Marekani vimewekwa katika kila sekta ya Iran wakati awali vilikuwa havihusu sekta zote. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuanzia mwaka 2010, nchi za Ullaya zilishirikiana moja kwa moja na Marekani katika kuiwekea vikwazo vikali sana Iran. Kwa maneno mengine ni kwamba, tangu mwaka 2010, Umoja wa Ulaya umekuwa ukishirikiana bega kwa bega na Marekani katika kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu kabisa

Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba lengo la Marekani ni kujaribu kulifanya taifa la Iran litengwe kieneo na kimataifa. Njozi ya Marekani ni kuwa, kwa kuizuia Iran kuingia kwenye mifumo ya fedha na biashara ya kimataifa, itaweza kubadilisha siasa za Iran. Lakini kama ilivyosema sehemu moja ya ripoti ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Bi Alena Douhan, wananchi na raia wa kawaida wa Iran ndio wahanga wakuu za vikwazo vya Marekani.