Sep 22, 2022 09:32 UTC
  • Iran yazindua kombora la balistiki la Ridhwan katika 'Wiki ya Kujihami Kutakatifu'

Kombora la balistiki la nchi kavu kwa nchi kavu lijulikanalo kama 'Ridhwan' la Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limezinduliwa katika gwaride la maadhimisho ya miaka 42 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini Iran ambalo limefanyika katika Haram Takatifu ya Imam Khomeini MA mjini Tehran.

Kombora la Ridhwan lina uwezo wa kulenga shabaha umbali wa kilomita 1400 na ni moja ya makombora ya kisasa kabisa ya IRGC.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, Kombora la Ridhwan limezinduliwa kwa mara ya kwanza kabisa katikwa gwaride hilo la leo.

Maadhimisho ya miaka 42 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini Iran yameanza leo asubuhi katika jiji na Tehran na miji mingine ya taifa hili.

Maadhimisho haya yameanza kwa mbwembwe za aina yake, ambapo mapema leo asubuhi vikosi tofauti vya Jeshi la Iran vimepiga magwaride hapa jijini Tehran na katika miji mingine ya Iran.

Mjini Tehran maadhimisho haya yanafanyika jirani na haram ya Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo viongozi wa serikali na makamanda mbalimbali wa ngazi za juu wa jeshi wameshiriki katika maadhimisho haya muhimu katika historia ya Iran.

Mkuu wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri

Ikumbukwe kuwa, Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Oparesheni za Iran za kukabiliana na uvamizi huo wa Saddam ni maarufu kama "Kujihami Kutakatifu".

Akizungumza katika gwaride ambalo limefanyika mjini Tehran, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri, amesema: "Kujihami kutakatifu kulionyesha ustahiki na fadhila za taifa la Iran ambalo pamoja na kuwepo hujuma ya maadui waliokuwa wakipata himaya ya uistikbari wa kimataifa, taifa la Iran liliweza kusimama kidete."