Sep 22, 2022 10:12 UTC
  • Rais wa Iran katika mkutano na Rais wa Finland: Wamagharibi wana undumakuwili kuhusu haki za binadamu

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na Rais wa Finland Sauli Niinistö na kusema undumakuwili wa madola ya Magharibi katika masuala ya haki za binadamu ni ukiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadmau.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini New York pembizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusu sera ya Tehran ya kustawisha uhusiano na nchi zote rafiki ikiwemo Finland.

Raisi amefafanua kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran na kusema, kwa kuzingatia kuwa Marekani na nchi za Ulaya zilizo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA zina historia ndefu ya kukiuka ahadi zao, leo hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kusema Iran haitumii mantiki wakati inapotaka dhamana kuwa nchi za Magharibi hazitakiuka tena ahadi zao katika mapatano ya nyuklia. 

Rais wa Iran aidha amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni vya kidhalimu na ni kinyume cha sheria na kuongeza kuwa: "Vikwazo ni muendelezo wa sera za uvamizi wa kijeshi kwa lengo la kulazimisha nchi zenye mitazamo huru kufuata matakwa ya madola ya kibeberu." Hata hivyo amesema vikwazo havijaweza kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kustawi. Aidha Rais Ebrahim Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa kipaumbele suala la kutetea haki za binadamu.

Kwa upande wake, Rais wa Finland amesema uhusiano wa Finland na Iran ni mzuri na unazidi kuimarika.