Sep 24, 2022 02:33 UTC
  • Kupungua ushawishi wa mfumo wa kambi moja; ulimwengu unakaribia kuingia katika mpangilio mpya wa utawala

Akizungumza karibuni katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Tumekusanyika hapa leo katika hali ambayo tunakabiliwa na ukweli muhimu, yaani, "kugeuka na kubadilika ulimwengu" na kuingia katika "zama na mfumo mpya."

Akizungumza siku ya Jumatano asubuhi kwa saa za Marekani, katika kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Seyyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia madhara na hatari ya mfumo wa utawala wa hivi sasa unaozidi kudhoofika duniani, na kubainisha juhudi kubwa ziazofanywa na taifa la Iran kwa ajili ya kupatikana mpangilio mwingine wa utawala uliosimama juu ya msingi wa haki na uadilifu duniani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Tumekusanyika hapa leo katika hali ambayo tunakabiliwa na ukweli muhimu, yaani, "kugeuka na kubadilika ulimwengu" na kuingia katika "zama na mfumo mpya." Ulimwengu wa zamani, umekuwa ni ulimwengu wa "mitazamo ya upande mmoja", "utawala wa ubeberu", "udhibiti wa ubepari dhidi ya maadili, uadilifu na wema", "unaoeneza umaskini, ubaguzi na dhulma", "matumizi ya mabavu, vikwazo na ukiukaji wa haki za mataifa" na "matumizi mabaya ya mashirika na taasisi za kimataifa" kama chombo cha kutoa mashinikizo dhidi ya nchi huru," na kwa neno moja, umekuwa ni ulimwengu usiozingatia usawa hata kidogo.

Raisi akizungumza karibuni katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kwa kutilia maanani kuwa hotuba katika Umoja wa Mataifa ni moja ya fursa chache ambapo walimwengu wanaweza kusikia sauti za nchi tofauti zilizo huru, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hotuba yake ya kwanza katika Baraza Kuu la umoja huo mwaka huu, amewajulisha walimwengu matokeo haribifu na hasi ya kuegemea misimamo ya upande mmoja kuhusu masuala ya amani, uadilifu na usalama katika maeneo tofauti ya dunia.

Dhulma na vurugu ni hali halisi ya dunia ya leo, ambapo hayo ni matokeo ya moja kwa moja ya kuegemea fikra za upande mmoja na hasa sera za Marekani na washirika wake wa Magharibi. Tathmini ya sera za Marekani katika miongo ya hivi karibuni inaonyesha kuwa nchi hiyo, haswa baada ya tukio la Septemba 11, ilizidisha vitendo na hatua zake za upande mmoja ulimwenguni na kisha kuishambulia Afghanistan baada ya kupita miezi michache.

Mwanzoni mwa shambulio hilo, Marekani haikukubali hata pendekezo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) la kutumia vifaa vyake na ushirikiano katika uwanja huo. Ilianzisha pia vita huko Iraq na Syria kwa visingizio visivyo na msingi kama vile kupambana na ugaidi, hali iliyopelekea maelfu ya watu kuuawa, na nchi hizo kushuhudia ukosefu wa utulivu, usalama na uwepo wa magaidi kwa miaka mingi.

Kuhusiana na hilo na katika kipindi cha utawala wa Donald Trump, Marekani ilianzisha mchakato wa kujiondoa katika taasisi na mapatano muhimu ya kieneo na kimataifa, kukiwemo kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kujitoa UNESCO, Mapatano ya Hali ya Hewa ya Paris, Makubaliano ya Ushirikiano ya "Trans Pacific" na Mkataba wa Anga Wazi.

Ni wazi kuwa, hatua za upande mmoja za Marekani zinazotekelezwa kwa zana za kijeshi na vilevile kuwekewa nchi huru vikwazo vikali vya kiuchumi kwa lengo la kufikiwa matakwa haramu  na yasiyo ya kisheria ya nchi hiyo si tu kwamba zimedhoofisha usalama wa kimataifa, bali pia zimeeneza dhuluma na kukiuka haki za binadamu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa dhulma hiyo, na wananchi wa Iran na vilevile nchi nyingine zisizofungamana na siasa za Marekani zimepata hasara kubwa kutokana na misimamo hiyo ya kuegemea upande mmoja na vikwazo vya kiuchumi vya miaka mingi. Suala hilo linaweka wazi udharura wa kufanyiwa mabadiliko mpangilio wa sasa wa Umoja wa Mataifa na kuanzishwa mfumo mpya wa kimataifa uliosimama juu ya msingi wa fikra za pande kadhaa. Kwa hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, Iran na nchi nyingine kubwa na zenye ushawishi barani Asia zimekuwa zikiimarisha uhusiano na maelewano ya pamoja kimataifa kwa msingi wa kuzingatiwa matakwa ya pande kadhaa kupitia taasisi muhimu za kimataifa kama vile Jumuiya ya Shanghai.

Marekani hutumia nguvu zake za kijeshi kuibua mivutano na ghasia duniani

Ni wazi kuwa sera za nje za Iran daima zimekuwa zikipinga kuegemea upande mmoja kifikra na kushiriki kikamilifu katika mashirika ya kimataifa yanayozingatia matakwa na misimamo ya pande ladhaa, na kutilia maanani uadilifu. Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuegemea upande mmoja unaochochea ukandamizaji, ndio tishio kubwa zaidi kwa jamii ya kimatifa na wala hakuna usalama utakaopatikana duniani  bila kuzingatiwa mfumo uliosimama juu ya msingi wa uadilifu.

Huku akisisitiza kuwa mfumo unaotawala sasa ulimwenguni si wa kiadilifu hata kidogo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Mfumo huu usio wa haki wala uadilifu umepoteza uhalali wake mbele ya fikra za waliowengi duniani na sasa kuna dhamira imara ya kutaka kuubadilisha. Kudhoofika na hatimaye kutoweka mfumo huo wa zamani ni jambo lisilo na shaka. Kanda yetu, yaani, Asia Magharibi, kutoka Afghanistan hadi Iraq, Lebanon, Palestina na Iran shupavu, ni jumba la makumbusho na dhihirisho la wazi la kupungua ushawishi na kutoweka taratibu mfumo huo wa zamani.