Sep 24, 2022 02:59 UTC

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, maadui walifanya njama kubwa za kuzuia kuwafikia walimwengu sauti ya taifa la Iran wakati wa ziara yake mjini New York Marekani alikohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana jioni mbele ya waandishi wa habari baada ya kurejea humu nchini kutoka New York Marekani na kuongeza kuwa, maadui walifanya kila wawezalo kuhakikisha sauti ya taifa la Iran haiwafikii walimwengu lakini sauti ya taifa la Iran ni sauti ya kuondolewa vikwazo vyote, ni sauti ya mashahidi waliouawa kidhulma kama Alhajj Qassem Soleimani, na ni sauti ya kupambana na dhulma na siasa za kindumilakuwili duniani. Amesema: "Mimi naamini kwamba maadui wameshindwa kufikia malengo yao."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia maandamano ya jana Ijumaa ya mamilioni ya wananchi wa Iran ya kulaani magenge yanayofanya uhalifu na fujo humu nchini waliochochewa na maadui wa taifa hili na kusema kuwa, kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika maandamano hayo kumezidi kusambaratisha njama za maadui.

Rais Ebrahim Raisi alirejea humu nchini jana Ijumaa akitokea New York Marekani alikohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

 

Amezungumzia pia jinsi nchi mbalimbali zilivyo na hamu ya kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema, hamu ya kustawisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na Iran kieneo na kimataifa inaonekana wazi duniani na leo hii kila mmoja analazimika kukiri umuhimu wa Jamhuri ya Kiislamu katika utatuzi wa matatizo ya kikanda na kimataifa. 

Vile vile amesema: "Sisi tunaamini kuwa, matatizo kama ya Yemen, Afghanistan na Ukraine hayana utatuzi mwingine isipokuwa mazungumzo tu."