Sep 24, 2022 06:56 UTC
  • Iran: Licha ya kwamba tuko chini ya mashinikizo makubwa, lakini tunaendelea kuhifadhi wakimibizi wengi

Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye pia ni mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika kikao cha 46 cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa "Kundi la 77+China" amesisitiza kuwa, Iran itaendelea kuwapa hifadhi wakimibizi licha ya vikwazo ilivyowekwa kwa miongo mingi sasa.

"Kundi la 77+China" jana Ijumaa lilitoa tamko la mwisho la kikao chake cha 46 na kuunga mkono misimamo ya Iran katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kupinga waziwazi hatua za upande mmoja za kiuchumi na kibiashara zilizochukuliwa na madola ya kibeberu dhidi ya Iran. 

Hivi sasa kundi hilo lina wanachama 134 na linahesabiwa kuwa ni kundi kubwa zaidi la kisiasa na kimazungumzo la Umoja wa Mataifa. Vikao vya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa kundi hilo hufanyika kila mwaka pambizoni mwa mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Is'haq Aal Habib, mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje na Mwakilishi wa Iran katika kikao cha 46 cha "Kundi la 77+China"

 

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Is'haq Aal Habib, mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje na Mwakilishi wa Iran katika kikao cha 46 cha "Kundi la 77+China" akisema hayo mjini New York Marekani na kuongeza kuwa, licha ya kuwa na matatizo yanayotokana na vikwazo vya kidhulma na haramu vya kiuchumi, lakini Iran inaendelea kuwahifadhi na kuwakirimu wakimbizi wengi wa kigeni, kuwapa elimu na mahitaji mengine yote ya lazima kama chakula, matibabu n.k.

Ameongeza kuwa,  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya juhudi kubwa za kusaidia kupatikana amani na usalama wa kikanda na kimataifa katika nyuga tofauti zikiwemo za kupambana na magendo ya mihadarati ambayo yameisababishia dunia hasara ya mabilioni ya dola.