Sep 24, 2022 07:13 UTC
  • Iran yajibu matamshi ya kifidhuli ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametumia mtandao wa kijamii wa Twitter kujibu matamshi ya kifidhuli ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliyejipa uthubutu wa kukosoa kile alichodai ni haki za binadamu nchini Iran.

Nasser Kan'ani Chafi ameandika katika ukurasa wake huo wa Twitter kwamba, Marekani ambayo ina historia ndefu ya aibu na ukatili kuhusu haki za binadamu, vipi inajipa uthubutu wa kutoa nasaha za masuala ya kimaadili na haki za binadamu kwa mataifa ya dunia?

Pia ameandika: Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje wa Marekani inabidi awe anaelewa kwamba katika kipindi cha miezi tisa tu ya mwaka huu, tayari polisi wa Marekani wameshaua kwa risasi watu 730 wa nchi hiyo na wengi wao ni Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Jumanne wiki hii pia, Kan'ani Chafi alijibu uingiliaji wa baadhi ya viongozi wa Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine waitifaki wao kuhusu kufariki dunia Mahsa Amini nchini Iran na kusema kuwa, nchi hizo zinajipa uthubutu wa kuingilia mambo yasiyozihusu katika hali ambayo zenyewe zimeoza kwa uvunjaji wa haki za binadamu.

Katika taarifa yake hiyo ya Jumanne, msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema pia kuwa, taifa zima la Iran limehuzunishwa na kifo cha mwananchi mwenzao Mahsa Amini, lakini cha kusikitisha zaidi ni kuona madola ya Magharibi yanatumia suala la haki za binadamu kama silaha ya kuyashinikiza mataifa yasiyokubali kuburuzwa.

Antony Blinken

 

Jana Ijumaa pia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliulaumu vikali utawala wa Kizayuni kwa uvunjaji wake mkubwa wa haki za binadamu na kusema kuwa, kitendo cha utawala wa kibaguzi wa Israel cha kutoka kwenye ukumbi wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Rais wa Iran alipokuwa anahutubia, hakiusaidii kitu utawala huo pandikizi na ukweli hauwezi kubadilika kwamba Palestina 'kutoka baharini hadi mtoni' ni mali ya wakazi wa asili wa ardhi hizo takatifu."

Mbali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kulaani vikali uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina alisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaamini kwamba, ardhi zote za Palestina ni nchi moja. "Utatuzi wa kadhia ya Palestina ni kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha wakazi wote wa asili wa ardhi hiyo, wawe Waislamu au Wakristo au Mayahudi kwa ajili ya kuamua mustakbali wa nchi yao."

Tags