Sep 24, 2022 07:25 UTC
  • Nafasi ya vikundi vya kifalme na vyombo vya habari vinavyopingana Uislamu katika machafuko ya sasa nchini

Katika siku za hivi karibuni, miji mbalimbali ya Iran imeshuhudia ukosefu wa usalama ambapo mkono wa waungaji mkono wa mfumo wa utawala wa kifalme na vyombo vya habari vya upinzani unaonekana wazi.

Maandamano ya kulalamikia masuala mbalimbali ni haki ya kiraia katika kila nchi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inaitambua wazi haki hiyo, lakini pamoja na hayo maandamano yanapogeuka na kuwa machafuko yanayopelekea watu kupoteza roho na mali zao bila sababu ya msingi, mambo huwa ni tofauti kabisa. Machafuko na ghasia si jambo linalofanywa na wananchi wa kawaida, bali ni maadui na wapinzani wa mfumo unaotawala ndio huzichochea na kutekelezwa na vibaraka wao wa ndani ya nchi wakiwemo baadhi ya watu waliopotoshwa na kuhadaika kifikra. Hali hiyo pia inaweza kuonekana wazi katika ghasia na machafuko yanayoendelea hivi sasa nchini Iran.

Makundi ya kifalme na wanafiki ni miongoni mwa makundi yanayoipinga serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na ambayo yanaona kuwa ndoto zao zimeambulia patupu baada ya kupita miaka 44 ya uhai wa Jamhuri ya Kiislamu na hivyo hulichukulia kila tukio linalotukia nchini kuwa fursa nzuri ya kuibua machafuko na ukosefu wa usalama nchini. Kuhusu matukio ya hivi karibuni, makundi hayo pia yametumia fursa ya vyombo vya habari vinavyopinga Jamhuri ya Kiislamu, hususan BBC na Iran International vya Uingereza na Saudi Arabia, kuchochea hisia za umma nchini Iran kwa lengo la kueneza maandamano na kuyageuza kuwa ya fujo na vurugu.

Baadhi ya uharibifu wa mali ya umma uliofanywa na magenge ya ghasia ya hivi karibuni

Kusimulia kichochezi maandamano hayo na kusambaza kwa wingi picha za magenge ya wachache wanaovunja sheria na kuwashambulia polisi ni ajenda kuu ya vyombo vya habari vilivyotajwa na vyombo vingine vya habari vinavyoshirikiana navyo kimawazo na kimalengo. Uharibifu wa mali ya umma ni sehemu ya mpango mkuu wa wanaounga mkono mfumo wa kifalme na ndio maana tukaona maeneo mengi ya serikali na umma yakishambuliwa na kuteketezwa na magenge ya wahalifu katika ghasia za karibuni.

Aidha katika ghasia hizo bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Qur'an Tukufu, msikiti na mitanndio ya kichwani ya wanawake wa Kiislamu zilichomwa moto pamoja na wanawake kadhaa waliopotoka kukata nywele zao hadharani, jambo lililoweka wazi ukweli kwamba ajenda inayofuatiliwa na makundi hayo sio kutetea haki za kijamii wala kiraia bali ni kupinga utawala wa kidini na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika muongo mmoja uliopita katika kupambana na ugaidi ambapo Munafiqeen wamekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na ugaidi huo, pamoja na mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kushinda siasa za mashinikizo ya juu kabisa za utawala wa Marekani, ambapo pia makundi hayo ya wanafiki yalikuwa na lengo kubwa la kuzifanikisha kwa madhumuni ya kuthibitisha ndoto yao ya kuupindua mfumo wa Kiislamu nchini, ni jambo lililoyakasirisha sana na hivyo kumua kuchochea na kufuatilia zaidi machafuko ya hivi sasa ndani ya nchi.

Jambo jingine muhimu ni kwamba machafuko hayo yameenda sambamba na kufanyika safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu mjini New York kwa lengo la kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Kwa hakika, kuathiri safari ya Raisi na kufanyika maandamano dhidi ya safari hiyo ya nje katika miji ya Magharibi, ikiwemo New York, na hatimaye kuigeuza kuwa lengo kuu la maswali ya vyombo vya habari kwa rais wa Iran ni moja ya malengo makuu yaliyofuatiliwa kwa karibu na waungaji mkono wa utawala wa kifalme na Munafiqeen nchini Marekani na maeneo mengine ya Magharibi.

Maandamano ya wananchi dhidi ya magenge ya vurugu nchini

Nukta ya mwisho ni kuwa, kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hivi karibuni, kusimama kidete mfumo wa Kiislamu mbele ya njama hizo kumewashangaza maadui, na kwamba mara hii pia maadui watashuhudia kufeli njama zao katika Iran ya Kiislamu. Katika kipindi cha miaka 44 iliyopita, wanachi shupavu na wapendwa wa Iran wamethibitisha kivitendo kwamba hujitenga na makundi ya ghasia na vurugu yanayoungwa mkono na vibaraka wa mfumo wa kifalme na Munafiqeen kwa ajili ya kuvunjia heshima thamani na matukufu ya kidini, na mara hii pia watazitenganisha safu zao na zile za maadui na wapinzani wa thamani za kidini.