Sep 25, 2022 03:07 UTC
  • Kan'ani Chafi: Iran haitasita hata kidogo kutoa jibu kwa uchokozi wowote ule

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haitasita hata kidogo kutoa jibu kwa uchokozi wowote ule.

Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo katika ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter katika majibu yake kwa matamshi ya kifidhuli ya Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na kubainisha kwamba, Waziri Mkuu wa utawala wa kigaidi nambari moja duniani alitumia jukwaa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kueneza chuki na kuwatishia watu wa Iran, akimwiga mtangulizi wake aliyeshindwa na kugonga mwamba katika mipango yake michafu.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, huu ndio mtindo na mbinu ya Wazayuni na washirika wao ya kuwatisha walimwengu na kisha kutaka wapatiwe kitu ambacho kimsingi siyo haki yao.

Nasser Kan'ani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Aidha msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, taifa hili limeshathibitisha kwamba, endapo litashambuliwa au kuvamiwa basi halitasita hata kidogo kutoa jibu kali na la kuogopesha.

Hayo yanairi katika hali ambayo, Jamhuri ya Kislamu ya Iran imetangaza mara chungu nzima kwamba, haitishwi na domokaya na bwabwaja za utawala ghasibu wa Israel na imejiandaa kikamilifu kujibu na kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote ile dhidi ya ardhi ya taifa hili la Kiislamu; na kama wanavyosisitiza viongozi wa Iran jibu la taifa hili litakuwa kali na kumfanya adui ajute.