Sep 25, 2022 06:48 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aonana na mawaziri wenzake wa Uganda, Eritrea na Imarati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana alionana kwa nyakati tofauti na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Uganda, Eritrea na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kubadilishana nao mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa. Mazungumzo ya mawaziri hao yamefanyika mjini New York, Marekani.

Katika mazungumzo yake na Haji Abubaker Jeje Odongo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Hussein Amir-Abdollahian ametilia mkazo wajibu wa kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano wa Tehran na Kampala katika nyanja zote.

Aidha katika mazungumzo yake na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea,  Osman Saleh Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, pande hizi mbili zina masuala mengi ya kuweza kuimarisha ushirikiano baina yao hasa kutokana na umuhimu wa maeneo ya Pembe ya Afrika na Ghuba ya Uajemi.

Mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uganda mjini New York Marekani

 

Hossein Amir-Abdollahian ameonana pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Sheikh Abdullah bin Zayed bin Sultan Aal Nahyan na kutilia mkazo siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuishi kwa usalama na amani na majirani zake na wajibu wa kushirikiana zaidi nchi za Waislamu bila ya kutoa fursa kwa madola ajinabi kuingilia masuala ya ndani ya eneo hili.

Amir-Abdolahian aliandamana na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika safari yake ya mjini New York Marekani ambako Rais Raisi alihutubia mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Tags