Sep 25, 2022 10:03 UTC
  • Amir-Abdollahian: Mwarubaini wa uvamizi Palestina ni kuitishwa kura ya maoni

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, tatizo la uvamizi na mzozo mkongwe katika Asia Magharibi litatuliwa kwa kutekelezwa ubunifu wa kidemokrasia wa Iran na kuitishwa kura ya maoni huko Palestina.

Hussein Amir-Abdollahian, amesema hayo katika mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nchi Wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), uliofanyika pambizoni mwa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kubainisha kwamba, kupitia kura ya maoni huko Palestina, wakazi wa asili wa ardhi hiizo wataainisha aina ya utawala wanaotaka.

Abdollahian amesema, inasikitisha kwamba, kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa na kigugumizi cha asasi za haki za binadamu ulimwenguni, hii leo Palestina inakabiliwa na hali mbaya.

Bendera ya Palestina

 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran ameashiria masuala kama uvamizi, kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina, mzingiro dhidi yao, uvamizi, mauaji na ukandamizajii wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel kama mifano ya wazi kabisa ya masaibu yanayowakabili wananchi wa Palestina huku jamii ya kimataifa ikiwa imeamua kukaa kimya.

Aidha amesema, utawala wa ubaguzi wa rangi wa Iisrael unawanyima kabisa Wapalestina haki zao za awali kama haki ya kuishi na kufanya kazi na badala yake unawalazimisha wayakimbie makazi yao kutokana na vitendo vya kinyama inavyowafanyia.

Abdollahi ameongeza kuwa, kuporwa ardhi za Wapalestina, kubomolewa nyumba zao na kujengwa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi ni sehemu nyingine ya vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Palestina.

Tags