Sep 26, 2022 03:35 UTC
  • Mabalozi wa Uingereza na Norway waitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Balozi wa Uingereza mjini Tehran ameitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kutokana na propaganda za kiuadui zinazofanywa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vya serikali ya London.

Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amemtaka Balozi wa Uingereza mjini Tehran, Simon Shercliff afike Wizara ya Mambo ya Nje kutokana na propaganda za kiuadui zinazofanywa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vya serikali ya Uingereza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, katika mkutano huo, balozi wa Uingereza amekabidhiwa hati ya malalamiko makali ya Iran dhidi ya serikali ya nchi yake inayosimamia vyombo vya habari ambavyo matangazo yao ya siku za karibuni yamejikita katika kufanya uchochezi na kuhamasisha fujo na uenezaji machafuko ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, suala hilo linachukuliwa kuwa ni sawa na kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sawa na kuchukua hatua dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya nchi.

Simon Shercliff

Balozi wa Uingereza amesema, atayafikisha malalamiko hayo London bila ya kuchelewa.

Wakati huohuo, balozi wa Norway mjini Tehran, naye pia ameitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kulalamikia misimamo ya spika wa bunge la nchi hiyo ya kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.

Sigvald Hauge ameitwa Wizara ya Mambo ya Nje kutokana na misimamo ya kiuingiliaji ya Masoud Gharahkhani, Spika wa Bunge la Norway, kuhusiana na matukio yanayojiri nchini Iran. 

Wakati wananchi wengi wa Iran wameguswa na kusikitishwa na kifo cha Mahsa Amini na hivi sasa wanasubiri kutangazwa matokeo ya uchunguzi wa sababu ya kifo chake, imefanyika mikusanyiko ya malalamiko na upinzani katika baadhi ya miji ukiwemo wa Tehran ambayo imesababisha uharibifu wa mali za umma.

Katika ghasia hizo, magari ya utoaji huduma, ya kubebea wagonjwa na ya Zimamoto nayo pia hayajasalimika na mashambulio ya wazusha machafuko na wavurugaji amani, kiasi kwamba hadi sasa mafundi kadhaa wa kada ya tiba na watoaji huduma za misaada wamejeruhiwa na kulazwa hospitalini, na magari 61 ya kubebea wagonjwa yameharibiwa.../