Sep 26, 2022 08:05 UTC
  • Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya awaunga mkono wafanya fujo nchini Iran

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ametangaza kuyaunga mkono makundi machache ya wananchi wa Iran wanaofanya fujo na kuharibu mali za umma na za watu binafsi kwa madai ya kulalamikia kifo cha Mahsa Amini binti wa Kiirani aliyeaga dunia hivi karibuni.

Josep Borrell ametoa madai hayo sambamba na kukaribia kikao cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja Ulaya chenye lengo eti la kujadili machaguo yote kwa ajili ya kuonyesha radiamali kuhusianan na kifo cha Mahsa Amini na namna vyombo vya usalama vya Iran vilivyoamiliana naye.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya hakuashiria kabisa vitendo vya uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi vinavyofanywa na wapinzani hao wachache wanaozusha fujo na machafuko na badala yake amesema kuwa, umoja huo unaamini kuwa, kutumia nguvu kupita kiasi kunakofanywa na vyombo vya usalama vya Iran ndiko kulikoongeza idadi ya wahanga wa maandamano nchini Iran.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya 

 

Wakati wananchi wengi wa Iran wameguswa na kusikitishwa na kifo cha Mahsa Amini na hivi sasa wanasubiri kutangazwa matokeo ya uchunguzi wa sababu ya kifo chake, imefanyika mikusanyiko ya malalamiko na upinzani katika baadhi ya miji ukiwemo wa Tehran ambayo imesababisha uharibifu wa mali za umma.

Katika ghasia hizo, magari ya utoaji huduma, ya kubebea wagonjwa na ya Zimamoto nayo pia hayajasalimika na mashambulio ya wazusha machafuko na wavurugaji amani, kiasi kwamba hadi sasa mafundi kadhaa wa kada ya tiba na watoaji huduma za misaada wamejeruhiwa na kulazwa hospitalini, na magari 61 ya kubebea wagonjwa yameharibiwa.