Sep 26, 2022 11:07 UTC
  • Kan'ani Chafi: Wanaojifanya watetezi wa haki za wananchi wa Iran wakomeshe vikwazo vyao vya miongo kadhaa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: wanaojidai kutetea haki za wananchi wa Iran wanapaswa waweke kando nara zao hizo za uongo na zilizochakaa, na badala yake wahitimishe vikwazo vya kidhalimu na vilivyo dhidi ya ubinaadamu walivyoliwekea taifa la Iran kwa miongo kadhaa.

Nasser Kan'ani Chafi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amekosoa mielekeo ya kiundumakuwili ya Marekani na Magharibi kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akaandika katika ukurasa wake wa Instagram kwamba: muekeleo wa maadui kuhusiana na Iran daima umekuwa ukichanganyika na unafiki na utumiaji vipimo vya undumakuwili; na akafafanua kwa kusema: "katika machafuko ya hivi karibuni, viongozi wa kisiasa wa Marekani na baadhi yao wa Ulaya, vyombo vyao vya habari, na vilevile vyombo vya habari vyenye uadui vya lugha ya Kifarsi vinavyoungwa mkono na nchi za Magharibi, havijaacha kufanya kila viwezalo ili kuwaunga mkono wafanya fujo na wavurugaji usalama wa taifa la Iran; lakini mkabala wake vyombo hivyo vimepuuza au hata kudogosha mahudhurio ya mamilioni ya wananchi wa Iran katika mabarabara na medani za nchi katika kuunga mkono Mfumo na nchi yao na kupinga vikali fujo na machafuko.
Uharibifu uliofanywa na wazusha fujo na wavurugaji usalama

Siku chache zilizopita, Kan'ani Chafi alijibu ujumbe wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken katika ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika: Marekani, ambayo ina rekodi ya kuaibisha ya haki za binadamu ndani na nje ya nchi, vipi inajipa uthubutu wa kujifanya iko juu kimaadili na kutoa nasaha kwa ulimwengu; Blinken inampasa akumbuke kuwa yeye ni waziri wa mambo ya nje wa nchi ambayo, ndani ya muda wa miezi tisa pekee, polisi wake wamewapiga risasi na kuwaua watu 730, wengi wao ni Wamarekani weusi". 

Katika upande mwingine, Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, ametoa matamshi ya uingiliaji masuala ya ndani ya Iran kwa kusema kwamba umoja huo unachunguza machaguo mbalimbali kutoa jibu kuhusiana na matukio yanayojiri Iran.
Borrell aidha amesema, sambamba na kukaribia kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, umoja huo utaendelea kufikiria machaguo yote iliyonayo kwa ajili ya kuchukua hatua kuhusiana na kifo cha Mahsa Amini na namna vyombo vya usalama vya Iran vinavyokabiliana na maandamano yaliyoibuka baada ya kifo cha msichana huyo.
Siku ya Alkhamisi ya tarehe 15 Septemba, Mahsa Amini alipelekwa kwenye kituo kimoja cha polisi cha hapa mjini Tehran kwa ajili ya kupatiwa maelezo na mafunzo, lakini akapata tatizo la moyo na kukimbizwa hospitalini mara moja kwa ushirikiano wa polisi na kitengo cha huduma za dharura, lakini kwa bahati mbaya akafariki dunia.../

Tags