Sep 27, 2022 07:41 UTC
  • Mkusanyiko wa mamilioni ya watu wa Iran; kufukuzwa wafanyaghasia na Umma wa Mtume Mtukufu (saw)

Wananchi wa mikoa tofauti ya Iran siku ya Jumapili, ambayo ilisadifiana na siku ya kukumbuka kifo cha Mtukufu Mtume (saw) na mkuu wake Imam Hassan Mujtaba (as), walifanya mkusanyiko wa mamilioni ya Umma wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ambapo walilaani vikali machafuko ya hivi karibuni nchini na pia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Wakati huo huo walitangaza wazi uungaji mkono wao mkubwa kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na matukufu ya kidini. Katika siku za hivi karibuni, maeneo mbalimbali ya Iran yameshuhudia ukosefu wa usalama na machafuko yaliyoanzishwa na wafanyaghasia na wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao mbali na kudhalilisha thamani za kidini na kitaifa hususan Qur'ani Tukufu na bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wameua na kujeruhi makumi ya watu.

Kidhahiri wafanyavurugu wametumia kisingizio cha kuwaunga mkono wanawake wa Iran katika maandamano hayo ya fujo, lakini walichokifanya kivitendo kinaonyesha kwamba kisingizio halisi cha ghasia hizo ni kupinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na thamani za kidini jambo limethibitishwa wazi na vitendo vyao vya kuchoma moto Qur'ani Tukufu, misikiti na bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia kutusi mfumo wa kidini unaotawala nchini.

Dhana potofu ya wafanyaghasia na waungaji mkono wao wa kigeni kwamba wangeweza kuhadaa watu na kuwafanya washirikiane nao kufikia malengo yao maovu kupitia nara tupu na za uongo kwamba wanaunga mkono haki za wanawake iliambulia patupu kufuatia mwamko wa wananchi wa Iran ambao katika kipindi cha miaka 44 iliyopita wamethibitisha mara nyingi kwamba:

Sehemu ya mkusanyiko wa mamilioni ya Waurani wanaounga mkono mdumo wa Kiislamu

Kwanza, wanatofautisha vizuri kati ya maandamano ya kupigania haki halali na fujo zinazochochewa na magenge ya ghasia na kamwe hawakubalini na fujo hizo.

Pili, licha ya kuwepo matatizo na mapungufu fulani, lakini bado wanaunga mkono kwa dhati mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na matukufu ya kidini.

Tatu, kukabiliana vikali na kisheria na wafanyaghasia, wanaovunjia heshima thamani za kidini na wanaoharibu mali za umma ni takwa kuu la wananchi.

Jumapili, watu wa Iran walionyesha wazi kuchukizwa kwao na wafanyaghasia na wanaotusi matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo kuthibitisha utiifu wao kwa mfumo na thamani za kidini kwa kuandaa mikusanyiko ya mamilioni ya watu katika mikoa tofauti. Mikusanyiko hiyo mikubwa imethibitisha kuwa, kile ambacho kimekuwa kikifanyika nchini katika siku za karibuni si maandamano ya kutetea eti haki za wanawake, bali ni njama ambayo imekuwa ikifanyika dhidi ya mfumo unaotawala nchini na thamani za kidini.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo taarifa iliyotolewa na mikusanyiko hiyo mikubwa nchini ikasema kwamba vitendo vinavyovunjia heshima matukufu ya dini na hasa kuchomwa moto Qur'ani Tukufu, misikiti na bendera ya Iran, kudhalilishwa vazi la stara la wanawake wa Iran ya Kiislamu pamoja na kuuawa shahidi walinzi kadhaa wa usalama, kunaonyesha wazi ukubwa wa njama na fitna zinazofanywa na maadui sugu wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa njama hizo za maadui wa kibeberu na Wazayuni zinatokana na chuki na uhasama wao mkongwe dhidi ya dini Uislamu, utukufu na mwamko wa Waislamu.

Suala jengine muhimu ni kwamba mikusanyiko hiyo ya mamilioni ya watu wa Umma wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) imewathibitishia maadui na wapinzani wa Kiislamu kuwa wananchi wa Iran wanapinga vikali harakati zozote zinazodhoofisha usalama na vikosi vya usalama nchini. Katika siku za karibuni, wafanyaghasia wameua shahidi au kujeruhi idadi kubwa ya jeshi la polisi na kufanya juhudi za kuharibu jina zuri la polisi mbele ya fikra za waliowengi nchini. Hata hivyo, mamilioni ya watu wamejitokeza na kushiriki katika mikusanyiko hiyo ambapo wametangaza hadharani uungaji mkono wao kwa jeshi la polisi, ambalo lina jukumu kubwa la kudhamini usalama ndani ya nchi.

Nukta nyingine ni kwamba mamilioni ya watu hiyo juzi waliwasilisha matakwa yao muhimu katika maandamano hayo ambapo walizitaka taasisi husika na mahakama kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaokiuka sheria na kuharibu mali za umma na za watu binafsi. Kwa hivyo, mikusanyiko mikubwa ya mamilioni ya watu katika mikoa na wilaya tofauti za Iran sio tu ilifanyika kwa ajili ya kulaani ghasia hizo, bali pia wananchi wametaka viongozi na watekelezaji wa ghasia na kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini wachukuliwe hatua zinazofaa kisheria.

Sehemu ya uharibifu uliofanywa na magenge ya vurugu na fujo nchini

Jambo la mwisho ni kwamba; moja ya nguzo muhimu za nguvu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni uungaji mkono wa wananchi na nguzo hiyo muhimu ilionekana wazi kwa mara nyingine tena katika maandamano na mikusanyiko mikubwa ya wananchi siku ya Jumapili. Ni uungaji mkono huo muhimu wa wananchi ndio umevunja njama na kuwakatisha tamaa maadui na wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 44 iliyopita. Katika hatua ya pili baada ya uungaji mkono huo wa wananchi, ni Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo kinyume na kile kinachoenezwa katika operesheni na vita vya kisaikolojia vya maadui, kuna matabaka tofauti ya wananchi, kuanzia kizazi cha kwanza cha Mapinduzi hadi kizazi cha wanafunzi walioko leo mashuleni, ambao kwa pamoja wameshikamana vilivyo na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na maadili yake, na wala malalamiko na maandamano yao kamwe hayana maana ya kupungua uungaji mkono wao kwa mfumo huo.