Sep 27, 2022 10:51 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amendelea na harakati zake za kidiplomasia pembeni mwa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kuonana na kufanya mazungumzo na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kuanzia wa mashariki hadi magharibi mwa Asia na kutoka Amerika ya Latini hadi Ulaya na Afrika.

Hossein Amir-Abdollahian ameonana na mawaziri hao pamoja na maafisa wa Umoja wa Mataifa njini New York na kutilia mkazo masuala mbalimbali yanayozihusu pande mbili, kieneo na kimataifa. 

Kwenye mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Mouritania, Bw. Ismael Ould Cheikh Ahmed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania amezungumzia njama za madola ya kibeberu za kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine ikiwemo Iran na kusema kuwa, lengo hasa la madola ya Magharibi ni kufuta matukufu ya Kiislamu na kupandikiza upotofu wao.

Vile vile amepokea vizuri fikra ya kuweko uhusiano wa kiistratijia baina ya Iran na Mauritania ikiwa ni pamoja na kwenye masuala ya Elimu ya Juu, Kilimo, Uvuvi na Nishati Jadidika.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea matumaini yake ya kuendelezwa mazungumzo, ufuatiliaji na utekelezaji wa maafikiano yanayofikiwa baina ya pande mbili ili nchi hizi mbili ndugu ziweze kuwa na ustawi mkubwa zaidi katika mahusiano yao.

Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiweki mipaka yoyote katika ustawishaji wa uhusiano wake na Mauritania. 

Akiendelea na harakati zake hizo za kidiplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonana pia na mawaziri wa mambo ya nje wa Belarus, Slovenia, Indonesia, Mali pamoja na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria na naibu wa Antonio Guterres katika masuala ya kibinadamu.

Tags