Sep 28, 2022 08:14 UTC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa undumakuwili wa Marekani ambayo inadai kuwa ina huruma na mapenzi na wananchi wa Iran, wakati ambapo imeliwekea taifa hili vikwazo shadidi.

Katika ujumbe wa Twitter jana Jumanne, Nasser Kanaani amewakosoa Wamagharibi kwa kuwaunga mkono wazusha fujo na machafuko yaliyoshuhudiwa kwa siku kadhaa sasa hapa nchini na kueleza kuwa, ni kinaya na fedheha kuona maafisa wa Marekani ambao walitaka kuwapigisha magoti wananchi wa Iran kwa mashinikizo ya kiwango cha juu na vikwazo vya kuumiza, kudai kuwa inatetea na kupigania haki za Wairani.

Amevikosoa vyombo vya habari vya Wamagharibi kwa kuchochea machafuko na fujo zinazoshuhudiwa hapa nchini kwa siku kadhaa sasa, kufuatia kifo cha binti wa Kiirani Mahsa Amini.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amekariri kuwa, muekeleo wa maadui kuhusiana na Iran daima umekuwa ukichanganyika na unafiki na utumiaji vipimo vya undumakuwili na kuwataka wahitimishe vikwazo vya kidhalimu na vilivyo dhidi ya ubinaadamu walivyoliwekea taifa la Iran kwa miongo kadhaa.

Maandamano ya kukosoa wafanya fujo Iran

Ali Bagheri Kaani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa pia amesisitiza kuhusu vigezo vya undumakuwili vinavyotumiwa na Umoja wa Ulaya kuhusu haki za binadamu na kuandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba: nchi za Ulaya ambazo zinakataa kuiuzia Iran dawa mbalimbali za matibabu na hivyo kusababisha vifo vya watoto wasio na hatia hapa nchini kwa namna ipi zinaweza kutiwa wasiwasi na suala la haki za binadamu nchini Iran? 

Jumapili iliyopita, watu wa Iran walionyesha wazi kuchukizwa kwao na wafanyaghasia na wanaotusi matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo kuthibitisha utiifu wao kwa mfumo na thamani za kidini kwa kuandaa mikusanyiko ya mamilioni ya watu katika mikoa tofauti. 

 

Tags