Sep 28, 2022 10:48 UTC
  • Iran: Jitihada za kufelisha kabisa vikwazo vya mabeberu zinaendelea

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, juhudi zinaendelea za kuhakikisha vikwazo vya mabeberu dhidi ya taifa hili la Kiislamu vinafeli na kutokuwa na athari yoyote.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kufikiwe makubaliano mazuri, imara na ya kudumu ambayo hayatoweza kutetereshwa kiurahisi.

Ameongeza kuwa, katika safari yake ya siku kadhaa huko New York Marekani alikokwenda kwa ajili ya kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, amefanya mazungumzo kadhaa rasmi na mawaziri wa mambo ya nje na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbalimbali kama ambavyo alionana pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na maafisa wengine kadhaa wa ngazi za juu wa umoja huo. 

Mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uganda mjini New York Marekani

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, katika mazungumzo yake hayo yote, amejitahidi kutangaza siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu na kuonesha hali halisi ilivyo hivi sasa katika eneo hili na duniani kwa ujumla pamoja na na kutilia mkazo wajibu wa kuangaliwa mambo katika uhalisia wake. 

Amma kuhusu mchakato wa mazungumzo ya kuondolewa Iran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa na Marekani, Amir-Abdollahian amesema, amezungumza na viongozi wa nchi mbalimbali na kuwabainishia wazi msimamo wa kimantiki wa Jamhuri ya Kiislamu ambao ni kupigania makubaliano mazuri, imara na ya kudumu ambayo yatakuwa na manufaa kwa wote.

Akiwa mjini New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipata fursa ya kuonana na kuzungumza na mawaziri wenzake wa nchi nyingi kuanzia wa mashariki hadi magharibi mwa Asia na kutoka Amerika ya Latini hadi Ulaya na Afrika.

Tags