Sep 29, 2022 11:57 UTC
  • Undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusiana na haki za binadamu nchini Iran

Huku Wamagharibi wakiendelea kuwachochea wananchi wa Iran kufanya ghasia na maandamano yenye uharibu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani misimamo na mienendo ya kindumakuwili ya nchi za Magharibi mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na haki za binadamu.

Nasser Kanani amesema: Ni mgongano wa kuaibisha kuona msemaji rasmi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi za Magharibi hususan Marekani ambayo imekuwa ikitekeleza sera za mashinikizo ya juu zaidi na vikwazo kwa ajili ya kuwapigisha magoti watu wa iran, wakijitokeza hadharani sasa na kujifanya walawalilia wananchi wa Iran!

Matamshi hayo ya Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran yanaashiria hatua na hujuma za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, hususan Marekani na Uingereza, dhidi ya Iran katika kipindi cha sasa, propaganda ambazo zinalenga kuchochea machafuko na ghasia nchini na bado zinaendelea kuwashawishi wanamichezo na wasanii kujiunga na ghasia na machafuko hayo.  

Japokuwa vyombo vya usalama na polisi ya Iran imefanikiwa kuzima fitina na machafuko ya siku kadhaa zilizopita yaliyoanzishwa kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini na eti kwa ajili ya kutetea haki za wanawake, na idadi kadhaa ya vinara wa machafuko hayo wametia nguvuni, lakini wanasiasa wa Magharibi na vyombo vyao vya habari ambao wana historia ndefu katika kukiuka haki za binadamu na kutekeleza sera za kindumakuwili katika suala hilo, wametumia machafuko ya karibuni hapa nchini kama kisingizio cha kuzidisha mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kudai kwamba wanatetea haki za watu wa Iran! 

Mfano wa wazi wa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusiana na suala la haki za binadamu ni kwamba sambamba na kifo cha Mahsa Amini nchini Iran, wanajeshi wa Marekani wapimpiga risasi na kumuua msichana Muiraqi, Zainab Essam huko magharibi mwa Baghdad; hata hivyo wanasiasa wa Magharibi na vyombo vyao vya habari vimenyamazia kimya na kufumbia macho kikamilkifu tukio hilo kiasi kwamba jina ya msichana huyu wa Kiiraqi limezikiwa pamoja na maiti yake.      

Zainab Essam alikuwa msichana mwenye umri wa miaka 15 ambaye aliuawa katika shamba la baba yake kwa risasi iliyofyatuliwa na wanajeshi wa Marekani, lakini cha kusikitisha ni kwamba, hata duru za haki za binadamu zinazohusishwa na Umoja wa Mataifa hazijazungumzia suala hili!

Mfano mwingine wa sera za kinafiki na kindumakuwili za nchi za Magharibi ni jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina ambazo zinarudiwa karibu kila uchao, na kila siku idadi kubwa ya Wapalestina wanauliwa, kujeruhiwa au kutekwa nyara, lakini waungaji mkono wa nchi za Magharibi wa utawala huo haramu na matarumbeta yao ya habari yanaendelea kunyamazia kimya uhalifu na jinai hizo.

Nukta nyengine muhimu ni kuwa, nchi za Magharibi sambamba na kudai kuunga mkono haki za wanawake, zinachochea machafuko na ghasia nchini Iran na kufumbia macho hali halisi na ya kusikitisha ya jamii zao, kwa sababu takwimu zilizopo zinaonyesha ukiukwaji mkubwa haki za wanawake katika nchi hizohizo za Magharibi.

Kwa mfano, katika utafiti uliofanywa na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Marekani, kwa uchache, mwanamke mmoja kati ya kila wanawake sita nchini Marekani amewahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono au ukatili katika utoto au utu uzima wao. Ripoti ya mwaka 2019 ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa pia ilieleleza kuwa wahanga 121 kati ya 149 wa ukatili wa majumbani nchini humo walikuwa wanawake. Ripoti hiyo ilisisitiza kuwa idadi ya wanawake walioaga dunia kutokana na ukatili huo iliongezeka kwa asilimia 28 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.

Ni wazi kwamba, sera za kinafiki na kindumakuwili za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya daima zimekuwa na athari mbaya zaidi kwa haki za binadamu. Nchi hizo zinazodai kutetea haki za binadamu ambazo zinahalalisha ukandamizaji wa waandamanaji, mauaji ya watu weusi, mauaji ya jamii za walio wachache hususan Waislamu, unyanyasaji na utesaji wa wafungwa na ukandamizaji wa wahamiaji ndani ya mipaka ya Ulaya, zinautambua utekelezaji wa sheria na hatua za kimahakama nchini Iran, ambayo iko chini ya vikwazo vya nchi hizo hizo, kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu na zinatumia ushawishi wa vyombo vyao vya habari kwa ajili ya kupindua ukweli.

Nasser Kanani

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran anaashiria ukweli huo akisema: Vyombo vya habari vya Wamagharibi na vikaragosi wao vinahamasisha mapigano ya mitaani na uharibufu wa mali ya umma na kuchochea migawanyiko ya kikabila na kikaumu, na wakati huo huo vinatoa nara ya "maisha kwa taifa la Iran"?!! Hakika ria na unafiki wa maadui wa taifa la Iran havina mwisho!