Sep 30, 2022 07:59 UTC
  • Amir-Abdollahian: Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alikuwa amebeba salamu za Marekani kwa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, katika kipindi cha miezi iliyopita baadhi ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi kadhaa wamekuwa wakifikisha jumbe za Marekani kwa Iran na kinyume chake, na akaongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein naye pia alikuwa amebeba ujumbe wa salamu za Marekani kwa Iran.

Katika mahojiano na shirika la habari la IRNA, Hossein Amir-Abdollahian amezungumzia pia mazungumzo ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pembeni ya mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, na kubainisha kuwa, katika mazungumzo hayo Macron kwanza alitaka kusikia mtazamo wa Iran kupitia ngazi ya juu ya rais na pili kubainisha rai na mawazo yake ambayo alihisi yanaweza kusaidia kupiga hatua na kufikiwa makubaliano.
Rais Ebrahim Raisi wa Iran (kulia) na Rais Emanuel Macron wa Ufaransa walipokutana New York

Kuhusu mazungumzo ya uondoaji vikwazo haramu ilivyowekewa Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu amesema, baada ya kutafakari, upande wa Marekani ulitoa maoni yake baada ya siku nane hadi tisa na katika baadhi ya masuala ambayo Iran ndiyo inayohusika zaidi, Marekani ilitoa maoni yanayoweza kutolewa tafsiri na kwa kiwango fulani yenye kuzusha utata katika hati ya mwafaka.

Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, Iran ina nia ya dhati ya kufikia makubaliano na haitaacha kufanya kila juhudi ili kuweza kufikia makubaliano mazuri, madhubuti na endelevu, wala haitaondoka kwenye meza ya mazungumzo na kwamba ni upande wa Marekani ambao inapasa uonyeshe kama unao ujasiri unaohitajika kwa ajili ya kuchukua uamuzi.../

 

Tags