Oct 01, 2022 05:23 UTC
  • Kamanda wa IRGC eneo la Sistan na Baluchestan auawa na magaidi

Kamanda wa kitengo cha usalama cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) katika mkoa wa kusini mashariki wa Sistan na Baluchestan ameuawa shahidi katika makabiliano na wapinga mapinduzi ambao walifyatua risasi karibu na msikiti katika mji mkuu wa mkoa huo, Zahedan.

Kufuatia shambulio la kigaidi kwenye kituo cha polisi cha Zahedan mapema siku ya Ijumaa, kundi la watu wenye silaha lilikusanyika karibu na msikiti wa Makki na kuanza kufyatua risasi, jambo ambalo lilifanya vikosi vya usalama kufika mara moja kwenye eneo la tukio.
Kamanda wa kitengo cha usalama cha IRGC katika mkoa huo, Ali Mousavi, alijeruhiwa kwa risasi kifuani na kupelekwa hospitalini. Hata hivyo alipoteza maisha alipokuwa akipata matibabu.
Gavana wa Sistan na Baluchestan Hossein Modarres Khiabani alisema takriban watu 19, wakiwemo maafisa wa polisi, waliuawa na 20 kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi katika kituo cha polisi eneo hilo.
Alisema, "wapiganaji kadhaa wenye mafungamano na makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga, ambao utambulisho wao uko wazi" walivamia kituo cha polisi na kurusha mawe na kufyatua risasi, jambo lililokabiliwa na jibu la polisi.
Magaidi hao pia waliteketeza gari la zima moto, kituo cha matibabu ya dharura, na benki, miongoni mwa maeneo mengine ya umma jijini lakini majaribio yao ya kuendelea na ghasia yalishindikana kufuatia kuwepo kwa vikosi vya usalama kwa wakati.
Katika taarifa, kundi la kigaidi la 'Jaish al-Zulm' limedai kuhusika na shambulio hilo huko Zahedan.

Tags