Oct 01, 2022 11:36 UTC
  • Mshikamano wa kitaifa, hitajio la kimkakati la leo la Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kile jamii inachohitajia sana hivi sasa ni umoja na mshikamano wa kitaifa kwa sababu maadui wanaulenga mshikamo wake wa kitaifa."

Rais Sayyid Ebrahim Raeisi Jumatano usiku alizungumza mubashara na wananchi kupitia televisheni na kubainisha namna adui anavyofanya hila ya kuibua mifarakano na kuvuruga umoja wa kitaifa hapa nchini na kuongeza kuwa: Hii leo wananchi wote wa Iran wako macho; na stratejia yetu muhimu zaidi ni kulinda mshikamano na umoja huo wa kitaifa. Hatupasi kivyovyote vile kutoa mwanya kwa adui kuvuruga mshikamano na umoja wetu wa kitaifa." 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha alisema, baadhi ya mauaji yanayofanywa na adui yanalenga kuvuruga umoja na mshikamano huu wa kitaifa; kwa msingi huo hii leo suala la mshikamano na umoja wa kitaifa ni jambo lenye umuhimu mkubwa na ni msingi wa taifa; jambo ambalo linapasa kutiliwa mkazo ili adui ashindwe kama ilivyo siku zote." 

Wananchi wa Iran wakiunag mkono serikali na kulaani ghasia na machafuko 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha wazi haya ambapo katika siku kadhaa za karibuni baadhi ya maeneo ya Iran yalikumbwa na ghasia na machafuko. Ghasia na fujo hizo ziliibuka kwa kisingizio cha kuuawa binti wa Kiirani kwa jina la Mahsa Amini hata hivyo maadui wa Iran ya Kiislamu walitumia suala hilo kama fursa ya kuibua mifarakano na migawanyiko katika jamii. Aidha maadui walijaribu kila wawezalo kuugombanisha mfumo na makabila na matabaka tofauti ya wananchi, wakiwemo wanafunzi, wasanii, wanariadha, walimu na wafanyakazi. 

Njama hizo za karibuni za maadui za kuibua mifarakano na migawanyiko na kutoa pigo kwa umoja wa kitaifa nchini Iran ziligonga mwamba na kufeli kufuatia juhudi za askari usalama na pia kuwa macho wananchi wa Iran. Hata hivyo matukio yote hayo kwa mara nyingine tena yamedhihirisha udharura wa kulindwa mshikamano wa wananchi. Umoja wa kitaifa ni msingi na mhimili mkuu wa kudumishwa umoja, uthabiti wa kisiasa na maendeleo ya jamii; na iwapo masuala hayo yatayumba basi sera zote za kiuchumi na kijamii zitasimama na hivyo kukwamisha maendeleo katika jamii. 

Ghasia za karibuni Iran 

Aidha wakati huu ambapo serikali na wananchi wa Iran wanakabiliwa na mashinikizo makali ya kisiasa na vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, suala la kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa lina umuhimu mkubwa kwa sababu ni kwa kudumisha umoja na mshikamano huu tu ndipo itawezekana kuendesha mapambano na muqawama na kuendeleza njia ya maendeleo katika jamii. 

Pamoja na hayo, inapasa kuashiria hapa kuwa kanuni na sheria za nchi zinatoa mwanya na kuruhusu watu wote kukosoa na kuandamana kwa amani madhali masuala hayo hayavurugi amani na kuhatarisha usalama wa taifa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza hili mara kadhaa. 

"Kujitawala na kuwa huru ni kauli kuu mbili za mapinduzi; na uhuru umedhaminiwa hapa nchini. Ndio, baadhi ya watu hawatendi haki, kwani wanatumia uhuru ulipo na kusema uwongo kwamba hakuna uhuru. Redio za maajinabi zinaakisi na kutangaza propaganda na yale yanayosemwa na watu hao. "Hii sivyo ilivyo, hii leo hapa nchini kuna uhuru wa kifikra, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kushiriki uchaguzi; hakuna anayeshinikiza, kutishwa au kubughudhiwa eti kwa sababu fikra na mitazamo yake inapingana na mtazamo wa serikali." (Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi tarehe 1 mwezi wa 1, mwaka 1397).  

Kwa hiyo, baadhi ya matukio yaliyojiri nchini katika siku za karibuni kwa kuchochewa na viongozi na vyombo vya habari vya adui; ambapo  magari ya kubebea wagonjwa, mabenki na hata askari usalama walishambuliwa hayapaswi kuitwa maandamano au harakati ya upinzani; hii ni kwa sababu vitendo kama hivyo ambapo mali za wananchi na usalama wa nchi unadhurika na kuwa hatarini katika nchi zote duniani huhesabiwa kama uzushaji fujo na ghasia na si maandamano ya kawaida.  

Katika hotuba yake hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia aliashiria na kusisitiza juu ya uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu kwa suala la kuanzisha jukwaa la kuwasilisha maoni na fikra huru na kusema: "iwapo mtu atakuwa na mawazo tofauti ya upinzani, hakuna tatizo, ana uhuru wa kubainisha mtazamo wake, lakini mtazamo ambao utakuwa ni wa kuwasilisha tu maoni na si kuibua fujo. Tunapasa tuache uwanja wazi kikamilifu kwa ajili ya kutolewa maoni yoyote ya upinzani, kukosoa na kuwasilisha malalamiko kwa ajili ya majadiliano, na  serikali hakika itaaminika katika uwanja huo."

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu