Oct 01, 2022 12:05 UTC
  • Raisi: Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na China katika kila uga

Rais Ebrahim Raisi wa Iran ametoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Jamhuri ya Kiislamu na China katika nyuga tofauti.

Sayyid Ebrahim Raisi ametoa mwito huo katika ujumbe aliomtumia Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jingping kwa mnasaba wa Siku ya Taifa inayoadhimishwa leo Oktoba Mosi nchini humo.

Katika ujumbe wake huo, Rais wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu na China kama mataifa mawili yanayopinga ubeberu na uingiliaji wa mambo yao ya ndani, yana fursa nyingi za kupanua uhusiano na ushirikiano wao.

Sayyid Raisi ameeleza kuwa, hakuna shaka kuwa irada ya kisiasa ya nchi mbili hizi ya kutekeleza hati za ushirikiano wa kistratajia inaweka wazi azma ya Tehran na Beijing ya kufikia maslahi ya pande mbili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: Dunia ya leo inakabiliwa na changamoto tele, na ili kupatia ufumbuzi matatizo hayo, kuna haja ya kuimarishwa ushirikiano wa mataifa huru na kutafuta suluhisho la pamoja la kimataifa.

Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kulitangazwa rasmi na Mao Tse Tung akachaguliwa kuwa rais wa jamhuri hiyo.

Kufuatia ushindi wa chama Kikomunisti mnamo Oktoba mwaka 1949, siku hii inatambulika kama Siku ya Taifa ya Jamhuri ya Watu wa China.

 

Tags