Oct 01, 2022 12:20 UTC
  • Jeshi la IRGC kutoa jibu kali kwa mamluki waliofanya mauaji ya kigaidi Zahedan

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limetoa taarifa ya kulaani shambulio la kigaidi lililopelekea makumi ya watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mji wa Zahedan, mkoani Sistan na Baluchestan kusini mwa Iran.

Kambi ya kijeshi ya Salman ya IRGC imesema katika taarifa leo Jumamosi kuwa, jeshi hilo litatoa jibu kali kwa magaidi waliohusika katika fujo na ghasia za umwagaji damu zilizoshuhudiwa hiyo jana mjini Zahedan.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, vikosi vya SEPAH vitashirikiana na vikosi vingine vya usalama, sera na intelijensia kutoa jibu kali kwa mamluki waliohusika na ghasia hizo, kwa lengo la kupanda mbegu za chuki na kufanya jinai.

Gavana wa Mkoa wa Sistan na Baluchestan kusini mwa Iran, Hussein Modarres Khiabani amesema watu 21 waliuawa huku wengine zaidi ya 20 wakijeruhiwa katika vitendo hivyo vya kigaidi vya hapo jana katika mji wa Zahedan, makao makuu ya mkoa wa Sistan na Baluchestan.

Alisema, wapiganaji kadhaa wenye mafungamano na makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga, ambao utambulisho wao uko wazi, walivamia kituo cha polisi na kurusha mawe na kufyatua risasi, jambo lililokabiliwa na jibu la polisi.

Kamanda wa kitengo cha usalama cha IRGC katika mkoa huo, Ali Mousavi, ni miongoni mwa watu waliouawa shahidi katika makabiliano na wapinga Mapinduzi ambao walifyatua risasi karibu na msikiti katika mji wa Zahedan.

Wakati huohuo, msemaji wa serikali ya Iran ameonya kuwa, ghasia na machafuko ni fursa nzuri kwa magaidi na mamluki kuhatarisha usalama na umoja wa wananchi wa Iran.

Baadhi ya silaha zilizonaswa mikononi mwa magaidi wazusha fujo Iran

Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa Twitter, Ali Bahadari Jahromi sambamba na kutoa mkono wa pole kufuatia kuuawa shahidi maafisa usalama na wakazi wa Zahedan amesisitiza kuwa: Ustawi wa taifa azizi la Iran umejengeka katika kivuli cha usalama. 

Wizara ya Usalama ya Iran imesema Marekani na Uingereza zimechochea ghasia zilizoshuhudiwa hivi karibuni kote Iran. Raia wa kigeni walionaswa wakichochea ghasia hapa Iran wana uraia wa nchi tisa zikiwemo Ujerumani, Poland, Italia, Ufaransa, Uholanzi na Sweden.