Oct 02, 2022 02:13 UTC
  • Mashambulizi ya IRGC dhidi ya ngome za magaidi huko Kurdistan Iraq

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetekeleza duru mpya ya mashambulizi dhidi ya ngome na maficho ya magaidi kufuatia kuongezeka hujuma na harakati dhidi ya Iran za magaidi waliopo katika eneo la Kurdistan huko Iraq.

Eneo la Kurdistan ya Iraq, kijiografia liko jirani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Eneo hilo limegeuzwa na kuwa mahali pa harakati za makundi ya kigaidi na yale yanayotaka kujitenga na Iran. Kwa upande mwingine, katika miaka ya karibuni, utawala wa Kizayuni umezidisha harakati zake za kuwepo na kujipenyeza katika eneo la Kurdistan huko Iraq. Kwa maneno mengine ni kuwa, maadui wawili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaani makundi ya kigaidi na utawala wa Kizayuni yamejizatiti katika eneo la Kurdistan huko Iraq huku yakiendesha harakati dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hali hiyo imeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ifuatilie kwa karibu zaidi yanayojiri katika eneo hilo la Kurdistan. Licha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuitanabahisha mara kadhaa serikali ya eneo ya Arbil na kuitaka ishughulikie changamoto za kiusalama zinazotishia amani ya Iran, lakini hadi sasa serikali hiyo ya eneo la Kurdistan haijatoa jibu lolote la kutuliza daghadagha na wasiwasi wa kiusalama ilionao Iran. 

Sambamba na hayo, baadhi ya matukio yanayojiri ndani ya Iran pia yanageuzwa na kutumiwa kama fursa ya kuendeshea harakati na hujuma za makundi ya kigaidi yanayoipinga Iran yenye makao yao huko Kurdistan ya Iraq. Makundi ya kigaidi kama Kumleh na Pijak ambayo yamejiimarisha pakubwa katika eneo la Kurdistan na vile vile yamejipenyeza ndani ya Iran yamehusika katika kuzusha fujo na machafuko hapa nchini. 

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, katika machafuko yaliyotokea katika siku za karibuni hapa nchini Iran magenge hayo ya kigaidi yenye makao yao Kurdistan ya Iraq yalihamasisha wafuasi wao ndani ya Iran, ambapo mbali na kuingiza silaha pia yalishiriki katika mpango wa kufanya mauaji na kuharibu mali za umma humu nchini.

Mbali na kufanya hujuma zote hizo, makundi hayo ya kigaidi hutoa mafunzo pia kwa vikundi vya wafanya fujo ndani ya eneo la Kurdistan; na baada ya kupatiwa mafunzo, wanachama wa vikundi hivyo huingia Iran na kuvuruga usalama wa taifa khususan katika maeneo ya mpakani mwa Iran. Harakati za magaidi wenye makao yao huko Kurdistan yakiwemo makundi ya Komleh na Pijak hazijajikita katika maeneo ya mpakani tu mwa Iran ambayo wakazi wake ni Wakurdi; bali zimeelekezwa pia hata katika maeneo ya katikati na kaskazini mwa nchi. Wafuasi wa makundi hayo waliojipenyeza ndani ya Iran wamekitumia kivuli cha maandamano ya malalamiko nchini, ili mbali na kuzusha fujo na machafuko kuwachochea pia wananchi wasimame dhidi ya mfumo wa utawala.

Magaidi wa eneo la Kurdistan, Iraq 

Kwa kuzingatia hali hiyo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limeanzisha duru mpya ya mashambulio dhidi ya magenge hayo ya kigaidi yenye yaliyoko katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Idara ya Uhusiano wa Umma ya vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Sepah imetoa taarifa na kutangaza kuwa, imetekeleza mashambulizi dhidi ya magenge ya kigaidi, baada ya kutoa indhari zinazohitajika kwa viongozi wa eneo la kaskazini ya Iraq za kuitaka ikomeshe harakati za makundi hayo ya kigaidi dhidi ya Iran na yenye mfungamano na mabeberu wa dunia katika eneo hilo na kutokana na kupuuzwa indhari hizo ilizotoa ambazo ni za haki na kisheria. Na sababu ya kufanya mashambulio hayo, ni kuendelea kuwepo magenge hayo katika eneo hilo la Kurdistan ya Iraq na kushambulia maeneo ya mpakani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zikiwemo baadhi ya kambi na vituo vyake vya kijeshi, mbali na kuchangia na kuunga mkono ghasia na machafuko ya hivi karibuni hapa nchini. 

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)

Taarifa ya vikosi vya nchi kavu vya Sepah imesisitiza kuwa, oparesheni hizo zitaendelezwa kwa nguvu zote hadi vitisho vilivyopo vitakapozimwa kikamilifu na ngome za magenge ya kigaidi zitakapoondolewa; na hadi pale viongozi wa eneo hilo watakapochukua hatua na kuwajibika ipasavyo katika uwanja huo.

Kwa maneno mengine ni kwamba, mashambulio ya SEPAH dhidi ya magenge ya kigaidi yenye makao yao katika eneo la Kurdistan ya Iraq ni hatua ya kulinda kisheria usalama wa taifa wa Iran na ya kupambana na ugaidi.

Tags