Oct 02, 2022 12:04 UTC
  • Mkutano wa Kimataifa wa Mshikamano na Watoto na Vijana wa Kipalestina wafanyika Tehran

Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Mshikamano na Watoto na Vijana wa Kipalestina umefanyika mjini Tehran.

Mkutano huo unafanyika katika kukumbuka mauaji ya Muhammad al-Durrah, kijana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 12, aliyepigwa risasi na mwanajeshi wa Israel mwaka 2000 mbele ya macho ya baba yake, umma na kamera za mashirika ya habari na kuuliwa kishahidi, alipokuwa amejificha nyuma ya baba yake ili kujikinga na risasi za askari wa Kizayuni.

Mkutano wa 5 wa kimataifa wa kuonesha mshikamano na watoto na vijana wa Kipalestina katika kumbukumbu ya mauaji ya Shahidi Muhammad al-Durrah umefanyika mjini Tehran ukihudhuriwa na wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), wanaharakati wa kimataifa wa masuala ya Palestina, pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu wa kanda ya nchi za Muqawama wa Kiislamu.

Akihutubia mkutano huo wa kimataifa Sayyid Mojtaba Abtahi, Katibu Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina ameashiria kuwa, miaka 22 imepita tangu kuuawa shahidi Muhammad al-Durrah, na kwamba tangu wakati huo muqawama na mapambano ya Palestina yamekuwa na rangi na mwelekeo tofauti.

Abtahi amesisitiza kuwa, baada ya kuuawa shahidi Muhammad al-Durrah gharama za kuiunga mkono Israel ziliongezeka kwa Marekani na madola ya Magharibi kwa ujumla, na utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa katika vita vingi licha ya uungaji mkono na madola hayo.

Katibu Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina amesisitiza kuwa, vijana wa Kipalestina ndio watawala wa baadaye wa ardhi hiyo na kusema: Kutokana na kizazi kipya kilichozaliwa katika nchi za Muqawama, kumeibuka milinganyo mipya katika eneo la Magharibi mwa Asia na hii leo umefika wakati wa ushindi wa mhimili wa mapambano katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.